Misingi ya Utume wa Kikristo, Mwongozo wa Mkufunzi

This is the Swahili edition of Capstone Module 4 Mentor Guide.

Jiwe Walilolikataa Waashi Limekuwa Jiwe Kuu la Pembeni

THE URBAN

Misingi ya Utume wa Kikristo

MINISTRY INSTITUTE huduma ya WORLD IMPACT, INC.

Mwongozo wa Mkufunzi

Moduli ya 4 Utume katika Miji

SWAHILI

MWONGOZO WA MKUFUNZI

Misingi ya Utume wa Kikristo

Moduli ya 4

Utume katika Miji

Maono na Msingi wa Kibiblia wa Utume

wa Kikristo: Sehemu ya Kwanza

Maono na Msingi wa Kibiblia wa Utume

wa Kikristo: Sehemu ya Pili

Utume wa Kikristo na Jiji

Utume wa Kikristo na Maskini

Mtaala huu ni matokeo ya maelfu ya masaa ya kazi iliyofanywa na taasisi ya The Urban Ministry Institute (TUMI) na haupaswi kudurufu bila idhini ya taasisi hiyo. TUMI inatoa idhini kwa yeyote anayehitaji kutumia vitabu hivi kwa ajili ya faida ya ufalme wa Mungu, kwa kutoa leseni za kudurufu za gharama nafuu. Tafadhali thibitisha kwa Mkufunzi wako ikiwa kitabu hiki kimepewa leseni ipasavyo. Kwa taarifa zaidi kuhusu TUMI na taratibu zetu za utoaji leseni, tembelea www.tumi.org na www.tumi.org/license .

Moduli ya 4 ya Capstone: Misingi ya Utume wa Kikristo – Mwongozo wa Mkufunzi ISBN: 978-1-62932-375-6 © 2005, 2011, 2013, 2015. The Urban Ministry Institute. Haki zote zimehifadhiwa. Toleo la kwanza 2005, Toleo la pili 2011, Toleo la tatu 2013, Toleo la nne 2015. © 2025 Kiswahili. Kimetafsiriwa na Samuel Gripper na Eresh Tchakubuta. Hairuhusiwi kunakili, kusambaza na/au kuuza vitabu hivi, au matumizi mengine yoyote pasipo idhini, isipokuwa kwa matumizi yanayo ruhusiwa kwa mujibu wa sheria ya Haki Miliki ya Mwaka 1976 au kwa idhini ya maandishi kutoka kwa mmiliki. Maombi ya idhini yatumwe katika maandishi kwa taasisi ya: The Urban Ministry Institute, 3701 E. 13th Street, Wichita, KS 67208. The Urban Ministry Institute ni huduma ya World Impact, Inc. Nukuu zote za Maandiko, isipokuwa kama imeonyeshwa vinginevyo, zimechukuliwa kutoka katika SWAHILI BIBLE UV050(MCR) series® Haki Miliki © 1997, iliyochapishwa na The Bible Society of Tanzania. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote za kimataifa zimehifadhiwa.

Yaliyomo

Muhtasari wa Kozi

3 5 9

Kuhusu Mkufunzi

Utangulizi wa Moduli

Mahitaji ya Kozi

17

Somo la 1 Maono na Msingi wa Kibiblia wa Utume wa Kikristo: Sehemu ya Kwanza

1

67

Somo la 2 Maono na Msingi wa Kibiblia wa Utume wa Kikristo: Sehemu ya Pili

2

123

Somo la 3 Utume wa Kikristo na Jiji

3

177

Somo la 4 Utume wa Kikristo na Maskini

4

229

Viambatisho

423

Kufundisha Mtaala wa Capstone

433

Maelekezo kwa Mkufunzi – Somo la 1

441

Maelekezo kwa Mkufunzi – Somo la 2

447

Maelekezo kwa Mkufunzi – Somo la 3

453

Maelekezo kwa Mkufunzi – Somo la 4

/ 3

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

Kuhusu Mkufunzi

Mchungaji Dkt. Don L. Davis ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya The Urban Ministry Institute na ni Makamu wa kwanza wa Rais wa World Impact. Alisoma katika Chuo cha Wheaton College na Chuo cha Uzamili cha Wheaton na kuhitimu kwa ufaulu wa kiwango cha juu, yaani Summa Cum Claude, katika ngazi ya Shahada (1988) na Shahada ya Uzamili (1989) katika Masomo ya Biblia na Theolojia ya Utaratibu. Alipata Shahada yake ya Uzamivu katika Masuala ya Dini (Theolojia na Maadili) katika chuo kikuu cha Iowa School of Religion. Akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi na Makamu wa Rais Mwandamizi wa World Impact , anasimamia mafunzo ya wamishenari wa mijini, wapanda makanisa, na wachungaji wa majiji, na kufanya uwezeshaji kupitia fursa za mafunzo kwa watendakazi Wakristo wa mijini katika uinjilisti, ukuaji wa kanisa, na umisheni wa upainia. Pia anaongoza Mpango wa Mafunzo huria kwa wale wanaosoma wakiwa mbali, vilevile anawezesha Mafunzo ya Kiuongozi kwa mashirika na madhehebu kadhaa kama Prison fellowship, The Evangelical Free Church of America na The Church of God in Christ. Dkt. Davis, ambaye ametunukiwa tuzo nyingi za ualimu na za kitaalamu, amewahi kuwa profesa na Mkuu wa vitivo katika taasisi kadhaa za kitaalamu zenye hadhi ya juu, baada ya kuhadhiri na kufundisha kozi za dini, theolojia, falsafa, na mafunzo ya Biblia katika taasisi za elimu ya juu kama vile Chuo cha Wheaton, Chuo Kikuu cha St. Ambrose, Programu ya Shahada ya Uzamili ya Theolojia ya Chuo Kikuu cha Houston, Kitengo cha Dini cha Chuo Kikuu cha Iowa, na Taasisi ya Mafunzo ya Ibada ya Robert E. Webber. Ameandika idadi kubwa ya vitabu, mitaala, na nyenzo za kujifunzia ili kuwaandaa viongozi wa mijini, ikijumuisha mtaala wa mafunzo wa Capstone (hii ni programu mama ya TUMI yenye moduli 16 za hadhi ya mafunzo ya seminari, yanayotolewa kupitia mfumo wa elimu ya masafa), Mizizi Mitakatifu: Kidokezo cha Namna ya Kurejesha Mapokeo Makuu , ambayo inaangazia namna makanisa ya mijini yanavyoweza kufanywa upya kupitia kugundua upya imani halisi, sahihi ya kihistoria; na Mweusi na Mwanadamu: Kumgundua Upya M.L. King kama Nyenzo ya Theolojia na Maadili ya Weusi . Dkt. Davis pia ameshiriki katika mihadhara ya kitaalamu kama the Staley Lecture series, makongamano ya kufanywa upya kama Promise Keeper Rallies na miungano ya kithiologia kama The University of Virginia Lived Theology Project Series. Vilevile alipokea tuzo ya heshima ya mwanafunzi mashuhuri ( Alumni Fellow Award ) kutoka Chuo Kikuu cha Iowa cha Sanaa na Sayansi za Kiliberali mnamo 2009. Dkt. Davis pia ni mwanachama wa The Society of Biblical Literature, na The American Academy of Religion .

/ 5

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

Utangulizi wa Moduli

Salamu, katika jina lenye nguvu la Yesu Kristo! Mada ya utume (umisheni) haijapewa mkazo na uzingativu upasao katika makanisa yetu ya mijini. Baada ya kuonekana kwa kiasi kikubwa kama kazi ya kuvuka bahari kwenda pembe za mbali za dunia, tumeshindwa kuipa uchambuzi wa kina na muhimu ambao inastahili. Kwa mtazamo wa upande mmoja, ukamilifu wa imani ya Kikristo unaweza kuonekana kama mwitikio wa utume, wito wa kwenda kwa mataifa na kumtangaza Yesu wa Nazareti kama Bwana na Mfalme wa utawala wa Mungu. Agano Jipya ni mkusanyo wa hati za kimishenari zilizotolewa kwa makanisa ambayo yalianzishwa na mitume, wamishenari wa awali wa imani ya Kikristo. Mungu mwenyewe ndiye mmishenari wa asili, aliyekuja ulimwenguni kwa njia ya Kristo na kuupatanisha ulimwengu na nafsi yake (2Kor. 5:18-21). Hakika, Ukristo ni utume. Kwa hiyo, moduli hii inashughulikia mada hii muhimu kwa nia ya kukusaidia wewe, kiongozi wa watu wa Mungu unayeandaliwa jijini, kuelewa theolojia ya utume na matokeo ya utume katika mtazamo wa kibiblia. Kwa maana halisi, hatuwezi kuelewa kile ambacho Mungu anafanya ulimwenguni kupitia utume bila kuwa na picha au muhtasari wa maono ya kusudi la Mungu na kazi yake. Kwa hiyo, katika masomo yetu mawili ya kwanza tutaangalia utume kupitia mitazamo minne tofauti: utume kama tamthilia na ahadi, na utume kama mapenzi na vita mtawalia. Katika somo letu la kwanza, Maono na Msingi wa Kibiblia wa Utume wa Kikristo (1) , tunashughulikia mtazamo wa utume (umisheni) kama Tamthilia ya Nyakati Zote. Nia yetu hapa ni kutoa mfumo wa kuielewa kazi ya utume kwa msingi wa Maandiko yenyewe. Tutaanza kwa kutoa ufafanuzi wa jumla wa utume, na kisha kuelezea muhtasari wa haraka wa vipengele muhimu vya ufahamu wa kibiblia wa utume. Tutaangalia utume kupitia mtazamo wa hadithi na tamthilia, tukionyesha kupitia Maandiko kwamba utume ni mamlaka kuu ya Mungu inayofanya kazi kupitia historia katika enzi au vipindi mbalimbali vya wakati ili kuleta ukombozi kwa njia ya Kristo. Pia tunaangazia utume kama utimilifu wa ahadi ya Mungu, tukiutazama utume kama utendaji wa Mungu katika kutimiza ahadi yake kama Mungu mwaminifu wa agano. Tutaelezea jukumu la maagano ya kibiblia katika Maandiko, na kufuatilia utendaji wa Mungu kama mwitikio wake kwa ahadi yake ya agano kwa Ibrahimu, iliyothibitishwa katika wanawe na mababa wa Taifa la Israeli, iliyohusishwa na kabila la Yuda na kufafanuliwa katika ahadi ya Mungu kwa Daudi ya kuwa na mrithi wa milele kwenye kiti chake cha enzi. Katika nafsi ya Yesu wa Nazareti, ahadi iliyotolewa kwa Ibrahimu na Daudi imetimizwa, na sasa,

6 /

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

kupitia utume wa kutangaza Injili, ahadi ya maisha mapya inatolewa kwa mataifa kupitia kuhubiriwa kwa Neno la msalaba. Katika somo la pili, Maono na Msingi wa Kibiblia wa Utume wa Kikristo (2) , tutachunguza utume kama Mapenzi ya Enzi na kama Vita vya Milki . Taswira hizi katika Maandiko zinatusaidia kuona jinsi utume ulivyo muhimu kwa theolojia yetu kama waamini. Kama Mapenzi ya Kiungu, tunaona azimio la Mungu la kuwatoa ulimwenguni watu ili wapate kuwa milki yake mwenyewe. Tutapitia mada hii muhimu, tukianza na historia ya Israeli kama mke wa Mungu, na taifa hilo lilivyokosa uaminifu kwa kugeukia ibada ya sanamu na kutotii. Tutafuatilia mada hii katika utu wa Yesu, na kuona jinsi agano jipya lilivyopanua wigo wa dhana ya “watu wa Mungu” ili kuwajumuisha Mataifa. Kama Vita vya Milki, tunaona tangazo la utawala wa ufalme wa Mungu kwa njia ya Yesu wa Nazareti. Tukianzia na uthibitisho wa wazi wa ukuu wa Mungu, tunaona kwamba Mungu ameamua kuweka upya utawala wake juu ya uumbaji wake, ambao ulianguka kutoka katika neema yake kupitia uasi wa shetani na wanadamu wakati wa Anguko. Tangu wakati huo, Mungu amechukua nafasi ya Shujaa ili kuurudisha ulimwengu chini ya utawala wake. Kwa njia ya Yesu wa Nazareti, Mungu anathibitisha tena haki yake ya kutawala ulimwengu mzima, na umisheni ni kutangaza ujio wa Ufalme huo kwa nji ya Kristo Yesu. Katika somo la tatu, Utume wa Kikristo na Jiji , tunaelekeza mawazo yetu kwenye lengo la utume na nia ya Mungu kwa ajili ya miji na watu maskini. Tunaanza kwa kuutazama mji wa kale, mpangilio wake na sifa zake, hasa sifa yake kama ishara ya uasi dhidi ya Bwana. Tutazingatia umuhimu wa kiroho wa jiji, tukiangalia namna Mungu alivyoshughulika na miji kadha wa kadha katika Maandiko, na kuchunguza maana ya mambo hayo. Tutaona jinsi ambavyo Mungu ameikubali dhana ya mji kwa makusudi yake mwenyewe, akibatilisha uhusiano kati ya dhana ya mji na uasi na ibada ya sanamu, na kuikomboa maana na msingi wa dhana hiyo kwa ajili ya utume, na kwa ajili ya utukufu wa Ufalme ujao. Hivyo, katika somo hili tutatoa mantiki ya kuhusika kwetu katika umisheni wa mijini. Jiji ni makao ya ushawishi, mamlaka, na shughuli za kiroho na vilevile sumaku inayowavuta walioonewa, waliovunjika moyo, na maskini. Kwa sababu hiyo, sisi kama wanafunzi wa Kristo katika karne ya 21, lazima tujitahidi kutamka matamko ya kinabii juu ya jiji na kuishi kinabii ndani ya jiji. Kama picha na ishara ya hatima na urithi wetu wa kiroho, lazima tufanye yote tuwezayo kuinjilisha watu, kufuasa watu (yaani kufanya watu kuwa wanafunzi wa Kristo), na kupanda makanisa katika miji yetu, ndani na nje ya nchi. Hatimaye, katika somo la nne tunachunguza kipengele kingine muhimu cha utume wa Kikristo. Katika somo hili liitwalo Utume wa Kikristo na Maskini ,

/ 7

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

tutachunguza dhana ya maskini na utume kupitia dhana tajiri ya kibiblia ya “shalom , ” au ukamilifu. Kama jamii ya agano ya Yehova, watu wa Israeli waliitwa kuishi kwa uaminifu katika agano la Bwana kwa kiwango ambacho kingesababisha umaskini uondolewe kupitia matendo ya haki na uadilifu. Akijenga juu ya tendo la ukombozi wake kwa watu wake kutoka Misri wakati wa tukio la Kutoka, Mungu aliwapa watu wake katika agano lake ramani ya mfumo wa haki ambao ungeshughulikia suala la umaskini na uonevu. Tukiwa na mtazamo huo wa Biblia, tutachunguza jinsi Yesu kama Masihi na Kichwa cha Kanisa anavyotimiza unabii wa Kimasihi kuhusu Yule ambaye angeleta haki na amani kwa maskini. Yesu kama Bwana na Kichwa cha Kanisa anaendelea kudhihirisha agizo la Mungu kwa ajili ya shalom kati ya watu wa Mungu, na kupitia watu wake, shalom ienee ulimwenguni. Kanisa, jamii ya agano jipya la Mungu kwa imani katika Yesu, limeitwa kuishi katika shalom na kuwaonyesha washirika wake na ulimwengu kwa ujumla haki ya Mungu kwa waliovunjika moyo. Hili linawezekana sasa kwa sababu ya Roho Mtakatifu anayewatia nguvu na kuwawezesha watu wa Mungu leo. Kama waaminio katika Yesu Kristo, kila mmoja wetu, kila kusanyiko limekombolewa ili tuweze kuwa watu wa ukombozi, kutangaza na kuiishi kweli ya Mungu pale alipotuweka. Kwa kweli, kuwa Mkristo ni kuwa na mwelekeo wa utume na kutengenezwa kwa ajili ya utume; tulizaliwa kutoka juu ili tuwe watenda kazi pamoja na Mungu katika utume wake wa kuvuna ulimwengu kwa ajili ya Mwanawe (Mdo. 9:15). Mungu na atumie kozi hii kukupa changamoto ya kufanya sehemu yako katika hadithi hii ya ajabu ya utukufu wa Mungu, na umisheni wake wa kuuleta ulimwengu kwake kwa njia ya Mwanawe na Mwokozi wetu, Yesu Kristo! - Mchungaji Dr. Don L. Davis

/ 9

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

Mahitaji ya Kozi

• Biblia (kwa madhumuni ya kozi hii, Biblia yako inapaswa kuwa tafsiri [mf. BHN, SUV, NEN, SRUV, au NIV, NASB, RSV, KJV, NKJV, n.k. ikiwa utatumia Biblia ya Kiingereza], na sio Biblia iliyofafanuliwa [mf. The Living Lible, The Message]). • Kila moduli katika Mtaala wa Capstone imeainisha vitabu vya kiada ambavyo vinatakiwa visomwe na kujadiliwa katika muda wote wa kujifunza moduli husika. Tunakuhimiza kusoma, kutafakari, na kufanya kazi husika pamoja na wakufunzi wako, wasimamizi, na wanafunzi wenzako. Kutokana na uhaba wa vitabu unaoweza kujitokeza kwa sababu kadha wa kadha (k.m., kushindwa kuchapisha vitabu vya kutosha), tunaweka orodha yetu ya vitabu rasmi vya Capstone vinavyohitajika kwenye tovuti yetu. Tafadhali tembelea www.tumi.org/books ili kupata orodha ya vitabu vinavyohitajika kwa ajili ya moduli hii. • Daftari na kalamu kwa ajili ya kuchukua maelezo na kufanyia kazi za darasani. • Erickson, Millard J. Introducing Christian Doctrine . Toleo la 2. Grand Rapids: Baker Book House, 2001. • Phillips, Keith. Out of Ashes . Los Angeles: World Impact Press, 1996. • Winter, Ralph D, and Steven C. Hawthorne, wah. Perspectives on the World Christian Movement: A Reader . Toleo la 3. Pasadena: William Carey Library, 1992. • Yohannan, K. P. Revolution in World Mission . Carrollton, TX: GFA Books (a division of Gospel for Asia), 2004.

Vitabu na Nyenzo Zingine Zinazohitajika

Vitabu vya Kusoma

1 0 /

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

Muhtasari wa Mfumo wa Kutunuku Matokeo na Uzito wa Gredi

Mahitaji ya Kozi

Mahudhurio na Ushiriki Darasani . . . . . . ....... 30% Majaribio . . . . . . . . . . . . . . . . ................. 10% Kukariri Maandiko. . . . . . . . . . . . . ............. 15% Kazi ya Ufafanuzi wa Maandiko. . . . . . . ........ 15% Kazi ya Huduma. . . . . . . . . . . . . .............. 10% Kazi za Usomaji na za Kufanyia Nyumbani . . ... 10% Mtihani wa Mwisho. . . . . . . . . . . . ............. 10%

alama 90 alama 30 alama 45 alama 45 alama 30 alama 30

alama 30 Jumla: 100% alama 300

Mambo ya Kuzingatia katika Utoaji Maksi

Kuhudhuria kila kipindi ni moja ya masharti ya msingi ya kozi hizi. Kukosa kipindi kutaathiri matokeo yako. Ikiwa una dharura isiyoepukika itakayokulazimu kukosa kipindi, tafadhali mjulishe mkufunzi wako mapema. Ukikosa kipindi ni jukumu lako kutafuta taarifa kuhusu kazi na mazoezi yaliyotolewa, na kuongea na mkufunzi wako pale inapobidi kufanya na kukabidhi kazi kwa kuchelewa. Sehemu kubwa ya mafunzo yanayohusiana na kozi hii hufanyika kupitia mijadala. Kwa sababu hiyo, unahimizwa na kutarajiwa kushiriki kikamilifu katika kila kipindi cha kozi hii. Kila kipindi kitaanza na jaribio fupi kuhusu mawazo ya msingi yaliyofundishwa katika somo lililopita. Njia nzuri zaidi ya kujiandaa na majaribio haya ni kupitia Kitabu cha Mwanafunzi na daftari uliloandikia maelezo ya somo hilo lililopita. Kukariri Neno la Mungu ni kipaumbele cha msingi kwa maisha na huduma yako kama mwamini na kiongozi katika Kanisa la Yesu Kristo. Kozi hii ina mistari ya Biblia michache, lakini yenye umuhimu mkubwa katika jumbe zake. Katika kila kipindi utahitajika kukariri na kunukuu (kwa mdomo au kuandika) mistari ya Biblia uliyopewa na mkufunzi wako. Neno la Mungu ni zana yenye nguvu ambayo Mungu anaitumia ili kuwaandaa watumishi wake kwa kila kazi ya huduma aliyowaitia (2 Tim. 3:16-17). Ili kutimiza matakwa ya kozi hii, lazima uchague kifungu cha Biblia na kufanya uchambuzi wa kina (yaani, eksejesia au ufafanuzi wa Maandiko). Kazi yako iwe na kurasa tano (ziliyochapwa kwa kuacha nafasi mbili kati ya mistari au kuandikwa vizuri kwa mkono), na kushughulikia moja ya theolojia na kanuni za msingi za utume wa Kikristo ambazo zimeangaziwa katika kozi hii. Ni shauku na matumaini yetu kwamba utashawishika kikamilifu na kuamini juu ya uwezo wa Maandiko

Mahudhurio na Ushiriki Darasani

Majaribio

Kukariri Maandiko

Kazi za Ufafanuzi wa Maandiko

/ 1 1

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

kuleta badiliko na athari chanya katika maisha yako na ya wale unaowahudumia. Unapoendelea kujifunza kozi hii, uwe huru kuongeza mistari kadhaa katika uchambuzi wako (takriban mistari 4-9) kuhusu jambo ambalo ungependa kujifunza kwa kina. Maelezo yote kuhusiana na kazi hii yametolewa katika ukurasa wa 10-11, na yatajadiliwa katika sehemu ya utangulizi ya kozi hii. Matarajio yetu ni kwamba wanafunzi wote watatumia mafunzo haya kivitendo katika maisha yao na katika majukumu yao ya kihuduma. Mwanafunzi atakuwa na jukumu la kufikiria namna ya kufanya mafunzo ya huduma kwa vitendo kwa kutumia kanuni alizojifunza katika mazingira halisi ya huduma. Maelezo ya namna ya kufanya mafunzo kwa vitendo yanapatika katika ukurasa wa 12, na yatajadiliwa katika kipindi cha utangulizi wa kozi. Mkufunzi wako anaweza kutoa kazi za darasani na kazi za nyumbani za aina mbalimbali wakati wa vipindi vya masomo au anaweza kuziandika katika Kitabu cha Mwanafunzi ulichonacho. Ikiwa una swali lolote kuhusu kile kinachohitajika kuhusiana na kazi hizi au muda wa kuzikusanya, tafadhali muulize mkufunzi wako. Ni muhimu kwa kila mwanafunzi kusoma maeneo yote ambayo inampasa kusoma katika vitabu husika vya kozi hii au katika Maandiko Matakatifu ili kujiandaa kwa ajili ya mijadala darasani. Tafadhali hakikisha unajaza na kukabidhi kwa Mkufunzi wako “Fomu ya Ripoti ya Usomaji” iliyomo katika Kitabu cha Mwanafunzi, kila wiki. Kutakuwa pia na fursa ya kupata alama za ziada endapo utasoma zaidi ya ulivyoagizwa. Mwishoni mwa kozi, Mkufunzi wako atakupa mtihani wa mwisho utakaofanyia nyumbani. Katika mtihani huu hautaruhusiwa kutumia vitabu vyako vya kozi hii isipokuwa Biblia. Utaulizwa swali ambalo litakusaidia kutafakari juu ya yale uliyojifunza katika kozi na namna yanavyoathiri mfumo wako wa fikra na utendaji wako katika huduma. Utakapokabidhiwa mtihani wa mwisho, mkufunzi wako atakupa taarifa zaidi kuhusu tarehe za kukamilisha na kukabidhi mtihani wako na kazi nyinginezo.

Kazi ya Huduma

Kazi za Darasani na za Nyumbani

Kazi za Usomaji

Mtihani wa Mwisho wa Kufanyia Nyumbani

Gredi za Ufaulu

Mwishoni mwa kozi hii, gredi zifuatazo zitatolewa na kuhifadhiwa kwenye mbukumbu za kila mwanafunzi: A – Kazi Bora D – Inaridhisha B – Nzuri sana F – Hairidhishi (Feli) C – Nzuri I – Isiyokamilika

1 2 /

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

Matokeo ya mwisho wa kozi yatatolewa katika mfumo wa gredi kwa kutumia skeli ya kutunuku matokeo kwa mtindo wa herufi zenye alama chanya na hasi, kisha alama za gedi yako ya ufaulu katika kazi mbali mbali zitajumlishwa na kugawanywa kwa idadi ya kazi na vipimo vingine husika ili kupata wastani wa matokeo yako ya mwisho. Kuchelewesha au kushindwa kabisa kukabidhi kazi zako kutaweza kuathiri matokeo yako. Hivyo, ni vyema kupangilia shughuli na muda wako mapema na kuwasiliana na mkufunzi wako endapo kutakuwa na changamoto yoyote. Kama sehemu ya ushiriki wako katika moduli hii ya Capstone iitwayo Misingi ya Utume wa Kikristo , utahitajika kufanya ufafanuzi (uchambuzi wa kina) wa mojawapo ya vifungu vifuatavyo vya Neno la Mungu kuhusu asili ya utume wa Kikristo na huduma ya mjini:  Mathayo 28:18-20  2 Wakorintho 6:1-10  Luka 4:16-22  2 Timotheo 4:1-5  Mathayo 5:13-16  Wakolosai 1:24-29 Madhumuni ya kazi hii ya ufafanuzi wa Maandiko ni kukupa fursa ya kufanya utafiti wa kina wa kifungu kimojawapo muhimu kuhusu asili na utendaji wa utume wa Kikristo. Kuona kwamba Mungu ni Mungu wa umisheni ni jambo la msingi kwa kila hatua ya huduma ya mjini; umisheni sio msisitizo wa msimu fulani wala kazi ya watu wachache wasio wa kawaida walio tayari kwenda ng’ambo kwa muda. Umisheni (utume), badala yake, ndio damu au kiini cha mtazamo wa ulimwengu wa Kiyahudi-Kikristo, moyo na roho ya utendaji wa Mungu duniani. Kwa maana moja, hadithi nzima ya Kikristo inaweza kuelezewa kama nia ya Mungu ya kuvuta kutoka duniani watu ambao watakuwa mali yake; umisheni ni kazi ya Mungu na kazi yetu. Madhumuni ya utafiti huu ni ili uweze kuchagua mojawapo ya maandiko hapo juu na kulitumia kama lenzi ambayo unaweza kuitumia kutafakari na kufikiria kwa kina kuhusu umisheni – msingi wake, utendaji wake, na umuhimu wake kwa uongozi wa Kikristo wa mijini. Unapojifunza mojawapo ya maandiko haya (au andiko lingine ambalo wewe na Mshauri wako mtakubaliana) tumaini letu ni kwamba utaangazia kipengele muhimu cha msingi wa umisheni wa Kikristo. Pia tunatamani kwamba Roho akupe ufahamu kuhusu jinsi unavyoweza kuhusianisha maana ya andiko hilo moja kwa moja na mwenendo wako binafsi wa ufuasi, na Kazi ya Ufafanuzi wa Maandiko (Eksejesia)

Dhumuni

/ 1 3

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

vile vile jukumu la uongozi ambalo Mungu amekupa kwa sasa katika Kanisa na huduma yako. Hii ni kazi ya kujifunza Biblia, na ili kufanya kazi ya eksejesia , ni lazima udhamirie kuelewa maana ya andiko husika katika muktadha wake. Ukishajua andiko lilimaanisha nini kwa wasomaji wake wa kwanza, unaweza kupata kanuni zinazotuhusu sisi sote leo, na kuzihusianisha kanuni hizo na maisha. Mchakato wa hatua tatu rahisi unaweza kukuongoza katika jitihada zako binafsi za kujifunza kifungu cha Biblia: 1. Je, Mungu alikuwa akisema nini kwa watu katika muktadha wa asili wa andiko husika ? 2. Ni kanuni gani ambazo andiko hili linafundisha ambazo ni kweli kwa watu wote kila mahali, ikiwa ni pamoja na sisi leo ? 3. Ni kitu gani Roho Mtakatifu ananiagiza kufanya kupitia kanuni hii, leo, katika maisha na huduma yangu ? Baada ya kuwa umeyajibu maswali haya katika kujifunza kwako kibinafsi, hapo sasa utakuwa tayari kuendelea kuandika ulichokigundua katika kazi uliyopewa . Angali hapa chini mfano wa muhtasari wa kazi yako: 1. Eleza kile unachoamini kuwa ndio mada kuu au wazo kuu la andiko ulilochagua. 2. Eleza kwa muhtasari maana ya andiko hilo (unaweza kufanya hivi katika aya mbili au tatu, au, ukipenda, kwa kuandika ufafanuzi mfupi wa mstari kwa mstari juu ya kifungu husika). 3. Eleza kanuni kuu moja hadi tatu au maarifa ambayo kifungu hiki kinatoa kuhusu Misingi ya Utume wa Kikristo. 4. Eleza jinsi kanuni moja, kadhaa, au zote zinaweza kuhusiana na yafuatayo:

Mpangilio na Muundo

a. Kiroho chako binafsi na namna unavyotembea na Kristo b. Maisha na huduma yako katika kanisa lako la mahali pamoja c. Hali au changamoto katika jamii yako kwa ujumla.

Kwa msaada au mwongozo, tafadhali uwe huru kusoma vitabu vya rejea vya kozi hii na/au vitabu vya mafafanuzi ( commentaries ), na kutumia maarifa yaliyomo katika vyanzo hivyo katika kazi yako. Unapotumia maarifa au mawazo ya mtu mwingine kujenga hoja zako, hakikisha unatambua kazi za waandishi husika kwa kutaja vyanzo vya taarifa hizo. Astahiliye heshima apewe heshima yake. Tumia marejeleo

1 4 /

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

ya ndani ya maandishi ( in-text-refences ), tanbihi ( footnotes ), au maelezo ya mwisho ( endnotes ). Njia yoyote utakayochagua kutaja rejea zako itakubalika, ilimradi 1) utumie njia hiyo moja katika kazi nzima, na 2) uonyeshe pale unatumia mawazo ya mtu mwingine, na umtambue mwandishi husika kwa kumtaja. (Kwa maelezo zaidi, angalia katika Kiambatisho cha Namna ya Kuandika Kazi Yako: Mwongozo wa Kukusaidia Kutambua Waandishi wa Vitabu vya Rejea ). Kabla hujakabidhi kazi yako, hakikisha inasifa zifuatazo: • Imeandikwa au kuchapwa vizuri na inasomeka na kueleweka. • Ni uchambuzi wa mojawapo ya vifungu hapo juu. • Imekusanywa kwa wakati (haijacheleweshwa). • Ina urefu wa kurasa 5. • Inafuata muhtasari au mpangilio uliotolewa hapo juu, na imeandikwa kwa namna ambayo msomaji ataweza kuelewa. • Inaonyesha jinsi kifungu husika kinavyohusiana na maisha na huduma leo. Usiruhusu maagizo haya yakuogopeshe; hii ni kazi ya kujifunza Biblia! Unachohitaji kuonyesha katika kazi hii ni kwamba ulisoma andiko husika, umeeleza kwa muhtasari maana yake, ukaweza kupata kanuni chache muhimu kutoka katika andiko hilo, na kuzihusianisha na maisha na huduma yako mwenyewe. Kazi ya ufafanuzi inabeba alama 45 na inawakilisha 15% ya jumla ya maksi zako, hivyo hakikisha kwamba unaifanya kazi yako kuwa bora na yenye maarifa ya kutosha ya Neno la Mungu. Neno la Mungu ni hai na linafanya kazi, na hupenya hadi kwenye kiini cha maisha yetu na mawazo ya ndani kabisa (Ebr. 4:12). Mtume Yakobo anaweka msisitizo zaidi juu ya kuwa watendaji wa Neno la Mungu, sio wasikiaji tu, tukijidanganya wenyewe. Tunahimizwa kulifanyia kazi, kulitii. Anaongeza kusema kwamba kupuuza nidhamu hii ni sawa na sisi kujitazama sura zetu za asili katika kioo na mara tunapoondoka tunasahau asili yetu (sis ni nani) na tulichokusudiwa kuwa. Katika kila hali, mtendaji wa Neno la Mungu atabarikiwa katika kila atendalo (Yak. 1:22-25). Shauku yetu ya dhati ni kwamba uweze kutumia maarifa unayojifunza kwa vitendo, ukiihusianisha elimu hii na masuala na mahitaji halisi katika maisha yako binafsi, Kazi ya Huduma

Utoaji Maksi

Dhumuni

/ 1 5

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

na huduma yako ndani ya kanisa lako na kupitia kanisa lako. Kwa hivyo, sehemu hii muhimu ya kukamilisha moduli hii itakuhitaji kubuni kazi ya huduma kwa vitendo ili kukusaidia kushirikisha wengine baadhi ya maarifa ambayo umejifunza katika kozi hii. Andiko la 1 Petro 2:9-10 linalielezea Kanisa kama taifa, ukuhani, na watu. Hakuna neno lolote kati ya haya linaloturuhusu kuuelewa wokovu wetu kama suala la mtu binafsi lisilohusiana na kusanyiko. Lengo la kazi hii ya huduma kwa vitendo ni kukusaidia kuimarisha ujuzi wako katika kuelezea uhusiano kati ya wokovu na Kanisa. Tafadhali kamilisha kila moja ya hatua zifuatazo: Tambua na uelezee kwa ufupi kwa maandishi hali fulani katika uzoefu wako wa zamani au wa sasa ambapo mtu unayemjua anadai kwamba hafikirii Kanisa kuwa ni sehemu muhimu ya maisha yake ya kiroho. (Unaweza kutumia jina la kubuni kwa ajili ya mtu huyu ikiwa ungependelea kuficha utambulisho wake). Namna hii ya kuliupuuzia Kanisa inajidhihirisha katika maneno yake; “Sijisikii kama ni lazima niende kanisani ili kumwabudu Mungu!” Au inaweza kujionyesha katika tabia yake; anadai kuwa ni Mkristo mzuri lakini mahudhurio yake kanisani ni ya mara chache sana. Andika mfano wa barua kwa mtu huyu ukianisha kwa maneno yako mwenyewe sababu ambazo zinakufanya uamini kwamba ameelewa vibaya kile ambacho Biblia inafundisha kuhusu wokovu na Kanisa. Maudhui ya barua hiyo yanapaswa kutokana na theolojia ambayo umejifunza katika kozi hii, na yaonyeshe ufahamu wako wa theolojia hiyo. Lengo la barua hii ni kuhamishia mawazo na dhana za kitheolojia katika uzoefu wa kivitendo. Hili si “andiko la kitheolojia,” bali ni wasilisho la mafundisho ya kibiblia ya kweli kwa mtu ambaye anaonyesha kuwa na uelewa potofu wa Maandiko au ameamua kwa makusudi kuyaasi Maandiko. Kabidhi nakala ya barua kwa mwalimu wako. Kisha, tafakari katika maombi ikiwa Mungu anaweza kukuruhusu umfikie mtu uliyeandika habari zake (ikiwa ni jambo lililopo sasa) na umtumie barua hiyo au kuzungumza naye ana kwa ana kuhusu wokovu wake na maisha ya kanisa. Kazi ya huduma inabeba alama 30 ambazo zinawakilisha 10% ya jumla ya maksi zako, hivyo hakikisha unashirikisha yale uliyojifunza kwa ujarisi na ripoti yako iwe yenye kueleweka vizuri.

Mpangilio na Muundo

Hatua ya Kwanza

Hatua ya Pili

Hatua ya Tatu

Utoaji maksi

/ 1 7

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

Maono na Msingi wa Kibiblia wa Utume wa Kikristo: Sehemu ya Kwanza

SOMO LA 1

ukurasa 433  1

Karibu katika jina la uweza la Yesu Kristo! Baada ya kusoma, kujifunza, kujadili, na kutumia maarifa ya somo hili, utaweza: • Kutoa muhtasari wa “ prolegomena ” (“neno la kwanza”) au “picha kubwa” kuhusu umisheni. • Kufafanua umisheni kama “tangazo la fursa ya wokovu na ukombozi wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo na kazi yake katika uwezo wa Roho Mtakatifu kwa makundi yote ya watu.” • Kutaja vipengele vya elimu ya kibiblia ya utume, ikijumuisha hitaji la ufahamu wa kina wa Mungu na makusudi yake kwa ulimwengu, kuhusianisha maelezo yote ya kihistoria katika mada moja, kuwa na mizizi katika Maandiko yenyewe, kujengwa juu ya msingi wa Yesu Kristo na kazi yake, na kuchukua kwa uzito njia ya kibiblia ya kujadili utume kupitia taswira, picha, na hadithi. • Kuelezea taswira nne au picha nne za kitheolojia za utume katika Maandiko, yaani, utume kama Tamthilia ya Nyakati Zote (Mungu kama mhusika mkuu katika hadithi kuu ya wakati wote); utume kama utimilifu wa ahadi ya Mungu (Mungu akitimiza ahadi yake ya agano kupitia Yesu Kristo), utume kama Mapenzi ya Enzi (Mungu kama Bwana-arusi wa jamii yake mpya ya wanadamu waliokombolewa); na Utume kama Vita vya Milki (Mungu kama Shujaa akianzisha tena utawala wake juu ya ulimwengu). • Kutoa muhtasari wa mambo makuu katika Tamthilia ya Nyakati Zote kwa mujibu wa awamu kuu za kusudi la Mungu linalofunuliwa, ikiwa ni pamoja na kipindi cha Kabla ya Wakati (ambacho kinaangazia uwepo wa Mungu kabla ya mwanzo na kusudi lake, siri ya kuasi na uasi wa mamlaka), Mwanzo wa Wakati (ambao ni pamoja na uumbaji wa ulimwengu na wanadamu, anguko na laana, protoevangelium [yaani tamko la kwanza la Injili], mwisho wa Edeni, kifo, na ishara za kwanza za neema), na Kufunuliwa kwa Wakati (ambako kunajumuisha ahadi kwa Ibrahimu, Kutoka, Kutekwa kwa Nchi, Jiji-Hekalu-Kiti cha Enzi, Utumwa na Uhamisho, na Kurudi kwa Mabaki).

Malengo ya Somo

ukurasa 435  2

1

1 8 /

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

• Kuelezea kukamilishwa kwa awamu za kusudi la Mungu linaloendelea kujifunua kuelekea Utimilifu wa Wakati (ambao ni pamoja na Kristo kuvaa mwili, kufunuliwa kwa Ufalme katika Yesu, mateso, kifo, ufufuo, na kupaa kwa Kristo); Nyakati za Mwisho (ni pamoja na kushuka kwa Roho Mtakatifu, kuanzishwa kwa Kanisa, kujumuishwa kwa Mataifa, na enzi ya utume wa ulimwengu), awamu ya Ukamilifu wa Wakati (ambayo inahusisha mwisho wa uinjilishaji wa ulimwengu, uasi wa Kanisa, Dhiki Kuu, Parousia , utawala wa Kristo duniani, Kiti Kikubwa cha Enzi Cheupe, Ziwa la Moto, na Kristo kukabidhi Ufalme kwa Mungu Baba), na hatimaye awamu ya Baada ya Wakati (ambayo inajumuisha mbingu mpya na nchi mpya, kushuka kwa Yerusalemu Mpya, nyakati za kuburudishwa, na kuingizwa kwa Enzi Ijayo). • Kufanya muhtasari wa maana za Utume kama Tamthilia ya Nyakati Zote : jinsi kusudi kuu la Mungu linavyoweka msingi wa historia yote ya mwanadamu, Mungu kama mhusika mkuu katika awamu za tamthilia ya kiungu zinazoendelea kujifunua, utume kama kurejesha kile kilichopotea mwanzoni mwa wakati, na kazi ya kufanya mataifa wote kuwa wanafunzi kama sehemu yetu katika kutimiza jukumu letu katika muswada (script) wa Mwenyezi Mungu . • Kutoa muhtasari wa vipengele vikuu vya Utume kama utimilifu wa ahadi ya Mungu, kwa kuanzia na ufafanuzi wa agano kama mkataba kati ya pande mbili, iwe watu binafsi, makabila, au mataifa; pamoja na kuwa na wajibu wa kutimiza masharti ya mkataba huo, na faida na manufaa kama matokeo ya kutimizwa kwa masharti hayo. • Kuelezea sifa kuu za kufanya agano katika Maandiko ikijumuisha jinsi walivyoitishwa na shahidi, walivyokuwa makini (yaani, kuvunja masharti ya mkataba kulionekana kama uovu mkubwa wa kimaadili), mkataba ulivyotolewa ushahidi kwa kutoa zawadi, kula chakula, na kuweka mawe ya ukumbusho, na ulivyothibitishwa kwa kiapo na kwa dhabihu. • Kutoa mifano kadhaa ya maagano katika Biblia, ikijumuisha agano la ndoa, agano na Nuhu, agano la Sinai na wana wa Israeli, ambayo yote yanazungumzia mkataba mzito kati ya watu binafsi, au kati ya Mungu na watu. • Kuchunguza taswira ya utume kama utimilifu wa ahadi ya Mungu iliyotolewa katika agano kati ya Mungu na Ibrahimu, pamoja na sharti lake la kwamba aondoke kutoka katika nchi yake na jamaa yake na kwenda katika nchi aliyoichagua Mungu mwenyewe, pamoja na baraka inayoambatana na

1

/ 1 9

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

sharti hilo kwamba Mungu angemfanya kuwa taifa kubwa, angembariki na kulikuza jina lake, kuwabariki wambarikio na kuwalaani wamlaanio, na kuzibariki jamaa zote za dunia kupitia yeye. • Kuangazia jinsi agano hilo la Abrahamu lilivyohuishwa, likathibitishwa kupitia Isaka na Yakobo, na kuhusishwa na Yuda kuwa kabila ambalo Masihi wa Mungu angetokea, na kuonyesha jinsi Uzao wa kifalme ulioahidiwa katika baraka za Abrahamu ungekuja kupitia agano la Mungu na Daudi na nyumba yake, ambaye mrithi wake angetawala milele juu ya nyumba ya Israeli na kuwa baraka kwa mataifa. • Kuonyesha jinsi ahadi hii ilivyotimizwa katika Yesu wa Nazareti, ambaye anawakilisha mfano halisi wa ahadi zilizotolewa kwa Ibrahimu na Daudi. Kupitia maisha yake, kifo, ufufuo, na kupaa kwake, ahadi ya agano ya Mungu imetimizwa. • Kueleza namna ambavyo utume ni kutangazwa kwa Habari Njema kuhusu uaminifu wa agano la Mungu, na Agizo Kuu kama jukumu la kutangaza ahadi iliyotimizwa kwa ajili ya wokovu wa wanadamu wote, kuanzia Yerusalemu, hadi miisho ya dunia. • Kuonyesha uhusiano uliopo kati ya jukumu la utume katika enzi hii na tamko la kwamba katika Yesu wa Nazareti ahadi iliyotolewa kwa Ibrahimu na Daudi imetimizwa, na sasa, kupitia utume wa kutangaza Injili, ahadi ya maisha mapya inatolewa kwa mataifa kupitia kuhubiriwa kwa Neno la msalaba. Rum. 16:25-27- Sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara, sawasawa na injili yangu na kwa kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na ufunuo wa ile siri iliyositirika tangu zamani za milele, 26 ikadhihirishwa wakati huu kwa maandiko ya manabii, ikajulikana na mataifa yote kama alivyoamuru Mungu wa milele, ili waitii Imani. 27 Ndiye Mungu mwenye hekima peke yake. Utukufu una yeye kwa Yesu Kristo, milele na milele. Amina. Labda hakuna kitu kinachovuta umakini kama vile misemo: “Hapo zamani za kale,” na ule unaoambatana nao kwa karibu: “Na wakaishi kwa furaha milele.” Tumepata kuisikia misemo hii – inawakilisha mwanzo na mwisho wa simulizi za hadithi, hekaya au ngano, hadithi ambazo wengi wetu tumezisikia tulipokuwa tukikua. Kusikia tu msemo “Hapo zamani za kale” kulitosha kabisa kutufanya “Kila wakati ni wakati wa hadithi” Hadithi ya Utukufu wa Mungu na Wito wa Utume

1

Ibada

ukurasa 435  3

2 0 /

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

tuache kuimba nyimbo zetu, tugeuze vichwa vyetu, na kutufanya tuvutiwe na kuanza kufikiria jinsi hadithi itakavyokuwa na mwisho wake utakuwaje. Kwa maana halisi, sisi sio tu viumbe wenye akili timamu, bali kama Socrates alivyowai kusema, (na kimsingi zaidi) sisi ni viumbe wanaosimulia hadithi; tunajielewa kulingana na hadithi tunazothamini, tunazosimulia, na hadhithi tunazojihusisha nazo. Hadithi ambazo tunazungumza juu ya taifa letu, familia zetu, na utu wetu ndio msingi wa uelewa wetu kuhusu utu wetu (yaani sisi ni nani), na pia ni msingi wa mambo tunayoshikamana nayo. Wahusika, mada, ploti (mtiririko wa matukio), na mandhari ya hadithi tunazosimulia hutengeneza mitazamo yetu wenyewe kuhusu maana ya ukweli, uadilifu na maadili ambayo tunakumbatia na kuyachukulia kama kanuni zinazoongoza maisha yetu. Kwa kweli, si jambo gumu kupata mtu, familia, ukoo, utamaduni, au taifa ambalo linajielewa kulingana na hadithi zao kuu ambazo zinabeba msingi wa falsafa zao, zinajenga maoni yao kuhusu historia, na kuunda mafungamano yao ya kijamii, kitamaduni, na kitaifa. Kwa njia fulani, tunaishi kulingana na hadithi ambazo tunasimulia, tunaamini, na ambazo tumewekea msingi wa maisha yetu. Msisitizo huu wa kawaida wa kijamii na kibinafsi juu ya jukumu la hadithi (bila kujali kwamba tunaziona kuwa hadhithi za kubuni au za kweli kihistoria) unaonekana kupotea kwa njia nyingi miongoni mwa wanaume na wanawake wengi wa Kanisa la leo. Katika makanisa yetu mengi tunaweka mkazo juu ya kweli za kinadharia, juu ya kanuni za imani na matamko ya imani, juu ya muhtasari mzuri na mfupi wa hadithi za Injili zilizochekechwa ili kupata sentensi chache ambazo ni rahisi kuhubiri au kufundisha ndani ya muda mfupi na hata kuzikariri kwa urahisi zaidi. Ingawa aina hii ya matumizi ya theolojia na kweli ya Kikristo inaweza kuwa na manufaa katika baadhi ya mahubiri na mafundisho, hasa kwa watu wachanga katika imani, kiini na msingi wa Injili umejikita katika hadithi ya Yesu ambayo haijafupishwa kwa “muhtasari safi.” Badala yake, imesimuliwa vyema kwa shauku, furaha, na mshangao tunapoangazia hadithi ya ajabu ya upendo mkamilifu wa Mungu unaoonyeshwa katika unyenyekevu wa ajabu wa Mwanawe kupitia tendo la kuvaa mwili, upendo wa kina ulioonyeshwa msalabani Kalvari, na ushindi mkuu ulioonyeshwa katika ufufuo wake na kupaa kwake mkono wa kuume wa Baba. Hakika, nguvu na neema ya Yesu Kristo haiwezi kupatikana katika kanuni na matamko ya imani peke yake; ni lazima ielezewe na kuigizwa tena na tena katika Neno na sakramenti. Ni asili ya imani ya Kikristo kusimulia hadithi hii na kuisimulia tena na tena. Tunaokolewa kwa kuing’ang’ania Injili na kutengeneza maisha yetu kupitia “Habari Njema” ambayo imekuwa “habari njema ya furaha kuu,” angalau kwa wale wanaoamini.

1

/ 2 1

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

Hivyo basi, haipaswi kuwa ajabu kwamba tunafafanua asili ya utume wa Kikristo kama kusimulia hadithi ya Yesu kwa wale wanaohitaji kuisikia. Umisheni daima umekuwa suala la kuchukua hatua ya kwenda kwa wale ambao hawajasikia Neno la upendo mkuu wa Mungu katika Yesu wa Nazareti na kuwasimulia hadithi hii kwa njia ambayo ni rahisi, ya wazi na yenye nguvu na ushawishi kwao. Kwa kuzingatia lugha yao, utamaduni wao, na kawaida zao za mawasiliano, tunatafuta kuifanya Injili ya neema ya Mungu iwe wazi katika muktadha wa utamaduni wao na jamii yao. Umisheni daima umekuwa kazi ya kusimulia hadithi ya utukufu wa Mungu katika Kristo tena na tena na tena. Lengo ni kwamba tuipeleke hadhithi hii mpaka miisho ya dunia ili kila watu wasikie, na wale wanaotubu na kuamini kweli ya hadithi hii wapate uzima wa milele. Kwa maneno ya moja kwa moja na ya wazi, hili linawakilisha mojawapo ya misingi mikuu ya utume wa Kikristo: kusimulia hadithi ile ya zamani ya Yesu na upendo wake. Kwa bahati mbaya katika duru kadhaa za Kikristo leo, wengi wameutupilia mbali ulimwengu wa Biblia ulioongozwa na hadithi, Injili ya Yesu, na mbinu ya utume inayotegemezwa na hadithi, huku wakikumbatia njia zenye mwelekeo wa kisayansi zaidi. Wakristo wengi wameacha nguvu ya hadithi na kufuata mbinu za kimantiki zaidi. Kwa hakika, katika baadhi ya makanisa yetu tumepoteza asili ya ajabu na yenye mguso inayotokana na usimulizi wa hadithi. Hadithi inaweka wazi ubora wa ukweli kwa njia ambayo maandishi ya kifalsafa au insha ya kisayansi haiwezi kamwe. Kwa kuweka msisitizo wao juu ya mahubiri ya ufafanuzi kwa kufuata mbinu za ufafanuzi zinazoaminika kisayansi ambazo zinakidhi vigezo vya ukosoaji wa kihistoria, waumini wengi wa Biblia wameiacha lugha yao ya asili na kukumbatia Injili kavu, ya kimantiki zaidi na isiyo na kina. Ingawa hawa wamechagua njia ya ulimwengu ili kuwasilisha ujumbe wa Injili, matokeo yamekuwa madogo na yasiyo na ushawishi. Kwa kukataa kusimulia hadithi, na kuisimulia vizuri, hatuushawishi ulimwengu wala hatuwi waaminifu kwa “lugha ya asili” ya Injili, ambayo ni kusimulia matukio ya kihistoria yahusuyo Kweli kwa njia ya hadithi ya Yesu wa Nazareti. Leland Ryken, kama wasomi wengine wachache wa kiinjili leo, anaangazia tabia ya Biblia ya kuzungumza kwa kutumia picha na hadithi badala ya lugha ya kiufundi. Anazungumza juu ya namna ambavyo tunakuwa wepesi kujiingiza katika makosa na kuteleza katika upepo wa kuona ujumbe wa Yesu kama muhtasari wa kitheolojia ulioambatanishwa na vielelezo: Kwa sababu ya Wakristo wengi kuichukulia Biblia kama kitabu tu kilichopo kwa makusudi ya kitheolojia na ibada, ni vigumu sana kutoingia kwenye kosa la kuitazama Biblia kama muhtasari wa kitheolojia wenye maandiko ya uthibitisho. Hata hivyo Biblia ni kitabu cha taswira na motifu (mada) zaidi kuliko kitabu cha dhahania na

1

2 2 /

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

nadharia. Ukweli huu umefichwa na jinsi wahubiri na wanatheolojia wanavyovutiwa kirahisi zaidi na nyaraka. Msomi mmoja wa Biblia amesema kwa usahihi kwamba Biblia inazungumza sana katika lugha ya picha. . . Hadithi, mifano, mahubiri ya manabii, tafakari za watu wenye hekima, taswira za wakati ujao, tafsiri za matukio yaliyopita, yote haya yanaelekea kuonyeshwa katika taswira zinazotokana na uzoefu. Mara nyingi hazitokei kwa lugha dhahania ya kiufundi. ~ Leland Ryken. Dictionary of Biblical Imagery . (toleo la kielektroniki). Downers Grove, IL: InterVarsity Press, 2000. Katika hadithi ya Injili picha za hadithi ya Mungu zinaonekana wazi wazi: Mwana Kondoo wa Mungu amewekwa juu ya mti kama dhabihu mbadala kwa ajili ya dhambi za ulimwengu. Kila mtu anayeamini kwamba huyu aliyekufa ni Kristo, kwamba alikufa na siku ya tatu akafufuka, atakombolewa kutoka katika dhambi zake, na kusamehewa adhabu yote mbele za Mungu, na kupewa Roho Mtakatifu ambaye atakaa ndani yake katika maisha haya yote, na kumfufua siku ya mwisho. Hadithi hii imerudiwa katika maisha ya mamilioni ya wanaume na wanawake, wavulana na wasichana, kwa zaidi ya miaka 2,000 ambao wanashikilia hadithi ya Yesu kama Habari Njema ya wokovu na uzima kwa watu wote. Umisheni unasimulia hadithi hii kwa watu wa ulimwengu, kwa lugha zao wenyewe, kwa njia ambazo wanaweza kuelewa na kuthamini upendo na neema ya Yule ambaye ni mwigizaji na mhusika mkuu wa hadhithi yake. Mungu ndiye Shujaa wa hadithi yake mwenyewe, na historia ya wokovu si kitu kingine chochote isipokuwa “Hadithi Yake”. Kwa imani, Hadithi ya utukufu wa Mungu inaweza kweli kuwa hadithi yetu wenyewe pale tunapoikumbatia. Ugunduzi upya wa kiini cha ujumbe wa Kikristo kama hadithi ni hitaji la lazima la wakati wetu, na ishara za theolojia mpya za “theolojia ya hadithi” na “theolojia simulizi” zinahitaji kurudi ili tupate kuelewa msingi wa uanafunzi na utume wa Kikristo. Msingi wa imani yetu ni hadithi kuhusu mhubiri mashuhuri Myahudi aliyedai kwamba Mungu ni Baba yake. Wale miongoni mwetu tunaoamini kwa hakika kwamba Yesu wa Nazareti alikuwa Masihi na Bwana wa wote tunashikilia hadithi hii kama tegemeo la maisha yetu, tumaini letu, na huduma yetu. Hebu tusisahau kamwe kwamba “Hapo zamani za kale” yetu hakika ina mwisho usemao: “Na wakaishi kwa furaha milele.” Kushiriki katika utume wa ndani na wa ulimwengu ni kutangaza hadithi hii, hadithi ya utukufu wa Mungu, kuishi kila siku papa hapa na sasa hivi mbele za Bwana anayeiandika kupitia sisi, mbele ya wale ambao bado hawajaisikia na kuielewa. Katika ulimwengu wa utume wa ulimwengu, kila wakati ni wakati wa hadithi.

1

/ 2 3

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

Baada ya kukiri na/au kuimba Kanuni ya Imani ya Nikea (iliyopo kwenye viambatisho), omba maombi yafuatayo: Utupe neema, ee Bwana, kuitikia kwa utayari wito wa Mwokozi wetu Yesu Kristo na kuwatangazia watu wote Habari Njema za wokovu wake, ili sisi na ulimwengu wote tupate kuuona utukufu wa kazi zake za ajabu; anayeishi na kutawala pamoja nawe na Roho Mtakatifu, Mungu mmoja, milele na milele. Amina. ~ Episcopal Church. Kitabu cha Maombi ya Pamoja na Utoaji wa Sakramenti na Ibada Nyingine na Sherehe

Kanuni ya Imani ya Nikea na Maombi

za Kanisa, Pamoja na Zaburi au Zaburi za Daudi. New York: The Church Hymnal Corporation, 1979. uk 215

1

Hakuna jaribio katika somo hili.

Jaribio

Hakuna Maandiko ya kukariri katika somo hili.

Mapitio ya Kukariri Maandiko

Hakuna kazi za kukabidhi katika somo hili.

Kazi za Kukabidhi

MIFANO YA REJEA

Mungu wa Historia na Tamthilia ya Mungu

Katika ulimwengu ambao unaona imani ya Kikristo kama chaguo la utashi binafsi (sio kama imani iliyojengwa juu ukweli wa kihistoria), Wakristo wengi wameacha kuitetea imani yao ya Kikristo kama imani ya kihistoria. Sehemu kubwa za mrengo wa kiliberali wa madhehebu makuu zote zimeikana “historia” muhimu ya madai ya Kikristo kuhusu Yesu. Kwa mfano, kundi la Semina ya Yesu ( the Jesus Seminar , yaani, ile kamati maarufu sana ya utafiti wa kisomi iliyopewa kazi ya kutambua ni maneno gani katika Injili zetu yanayosemekana kwamba ni maneno ya Yesu, ambayo kwa kweli aliyasema Yesu mwenyewe), kamati hii ilidai kuwa iliweza kupata maneno machache tu yaliyotawanyika huku na kule, ambayo kamati ilikuwa tayari kusema kwa hakika labda ni habari sahihi za kihistoria kuhusu Kristo. Seminari nyingi zimechagua “utafiti wa kisayansi wa dini” ambao hauangazii kile ambacho Wakristo wameshikilia na kuamini katika karne zote, bali unaangazia kile ambacho sayansi inaweza kuthibitisha sasa kwa msingi wa uwezo wake wa kuthibitisha madai ya Ukristo. Mashambulizi haya na mengine yamefanya iwe vigumu kwa wengi kuukubali Ukristo kama hoja ya kihistoria isiyo

1

2 4 /

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

na mashaka, halika linakuwa jambo gumu kuuchukulia ufufuo kama ukiri wenye ukweli ndani yake. Kwa nini unafikiri ni muhimu kwa kazi ya umisheni kila mara kuanza na ufahamu wa kihistoria wa imani ya Kikristo kabla ya kuanza kuzungumza juu ya kipengele cha umisheni cha kuwashirikisha wengine imani hiyo? Kwa nini maoni ya Paulo kuhusu ufufuo kama msingi wa mahubiri na mafundisho yote ya kweli kuhusu Kristo hayaruhusu wala kutoa nafasi kwa maoni yoyote ya Ukristo ambayo yanakataa kukumbatia thamani ya ukweli wa kihistoria wa hadithi na Injili yetu? Wakati ambapo Hollywood inalipuka kwa filamu za hekaya na hadithi nzito nzito ( Gladiator, The Lord of the Rings, The Chronicles of Narnia , n.k.) mimbari nyingi za Kikristo zimesalia zikiwa zimefungwa kwenye muundo wa kutunga hotuba na uwasilishaji wa mahubiri katika mfumo wa «vipengele vitatu, shairi, na maombi.» Aina hii ya mahubiri na uwasilishaji inaonekana kupuuza nguvu ya hadithi katika jamii yetu kwa ujumla. Kwa sababu ya kuhangaikia zaidi kutoa “uthibitisho” wa Ukristo na utetezi wa “ushahidi unaodai uamuzi,” wafafanuzi na wahubiri wengi wa Kikristo wameacha kuisimulia Hadithi Kuu kama msingi wa huduma na utume wa Kikristo. Katika jitihada za kufikia na kugusa mioyo na akili za wale waliozoea mahubiri katika zama za kidijitali, wengi wameacha lugha ya asili ya Biblia kuhusiana na taswira, unabii, ushairi, na hadithi na kukumbatia zaidi mafundisho yanayohusu masuala ya “kisasa”, masuala ya maadili na mabadiliko ya kijamii kuliko kujishughulisha na aina za hadithi ambazo Hollywood kadhalika Biblia inasisitiza zaidi. Unadhani kwamba mkazo wa kisasa wa mafundisho kuhusu maadili ya kijamii na mihtasari ya moja kwa moja ya kitheolojia ni kusoma vibaya utamaduni? Je, unaamini nini—utamaduni unatafuta hadithi ambayo inaweza kuvuta usikivu na kuongoza mitazamo yake au maelezo ambayo yanaweza kutatua matatizo yake? Eleza. Je, Tunasoma Vibaya Alama za Utamaduni?

1

2

Hakuna Anayetimiza Ahadi Zake Siku Hizi

Wakati ambapo katika jamii kwa ujumla imekuwa nadra watu kuchukulia ahadi zao kwa uzito, tufanye nini ili hadithi ya ahadi ya Mungu iweze kuwa wazi na ya kuaminika? Katika jamii yetu ya leo, ahadi zinatolewa na kuvunjwa kwa urahisi wa ajabu sana: ahadi za ndoa zinaishia kuwa talaka za kutisha zenye kusababisha matengano, wanasiasa wanakula kiapo cha kulinda majimbo yao kisha baadaye wanashikwa katika ufisadi na unyanyasaji, wahubiri wanalia machozi ya mamba huku wakikiri majuto yao kwa sababu ya (kushikwa?) aibu na kashfa zao ambazo

3

/ 2 5

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

sasa ni mada za matangazo ya redio ya usiku wa manane. Inaonekana leo kwamba ni watu wachache sana wenye tabia ya kutimiza ahadi au kuthamini nguvu ya ahadi iliyoiweka. Hata hivyo, hadithi nzima ya imani ya Kikristo ina mizizi katika uwezo wa kutambua jinsi ahadi ya Mungu kwa habari ya Mwokozi ilivyokuwa muhimu, na jinsi ahadi hiyo ilivyotimizwa kupitia Yesu wa Nazareti. Je, mmomonyoko huu wa uadilifu katika utoaji na utimizaji wa ahadi katika jamii yetu unaathiri vipi uwezo wetu wa kuelewa asili ya imani ya Kikristo, na pia kufanya huduma na utume katika jamii kama yetu? Je, unafikiri kwamba ukosefu wa uadilifu katika jamii yetu unaathiri uwezo wetu wa kuelewa na kuthamini uadilifu wa Mungu katika Injili, yaani wokovu ambao ametupatia katika Kristo? Eleza.

1

Maono na Msingi wa Kibiblia wa Utume wa Kikristo: Sehemu ya Kwanza Sehemu ya 1: Utume kama Tamthilia ya Nyakati Zote

YALIYOMO

Mchungaji Dkt. Don L. Davis

Utume ni tangazo la fursa ya wokovu na ukombozi wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo na kazi yake katika uwezo wa Roho Mtakatifu kwa makundi yote ya watu . Ukitazamwa kama tamthilia na hadithi ya Mungu, kutoka Kabla ya Wakati hadi Baada ya Wakati , tunaweza kuanza kuona jinsi ambavyo katika hadithi ya utume, Mungu wa Utatu anatenda kazi kama Mungu Mwenye Enzi Kuu , akitenda kazi katika mambo yote kwa utukufu wake na manufaa yetu. Lengo letu katika sehemu hii, Utume kama Tamthilia ya Nyakati Zote , ni kukuwezesha kuona kwamba: • Neno “ prolegomena ” linamaanisha “neno la kwanza,” na p rolegomena juu ya utume lazima ianze na mtazamo wa kibiblia wa ulimwengu juu ya Mungu na kazi yake duniani kupitia Yesu wa Nazareti. • Utume unaweza kufafanuliwa kama “tangazo la fursa ya wokovu na ukombozi wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo na kazi yake katika uwezo wa Roho Mtakatifu kwa makundi yote ya watu.” • Uelewa wa kibiblia wa utume una vipengele fulani ambavyo vinaweza kubainishwa kutokana na usomaji wa Maandiko yenyewe. Utume lazima ujengwe juu ya msingi wa ufahamu sahihi wa Mungu na makusudi yake kwa ulimwengu, kuhusianisha maelezo yote ya kihistoria katika mada moja. Mtazamo wa kibiblia wa utume, pia, lazima ujikite katika Maandiko

Muhtasari wa Sehemu ya Kwanza

Made with FlippingBook - Online catalogs