Mungu Baba: Swahili Module 6 Mentor Guide
/ 5
M U N G U B A B A
Utangulizi wa Moduli
Salamu, wapendwa marafiki, katika Jina lenye nguvu la Yesu Kristo! Somo la nafsi ya Mungu wetu, Baba Mwenyezi, ni moja ya masomo muhimu na ya thamani sana kuliko masomo yote katika Neno la Mungu. Somo hili linaathiri kila nyanja ya ufuasi wetu, ibada, na huduma; hakika, ni kama Bwana wetu Yesu alivyosema, “Na uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma,” (Yohana 17:3). Katika somo letu la kwanza, Prolegomena: Fundisho kuhusu Mungu na Kuenea kwa Ufalme , tutachunguza kwa ufupi mambo ya kwanza, prolegomena , ambayo ni msingi wa theolojia, huku tukiangalia umuhimu wa Mungu kujifunua kwetu. Tutajifunza dhana za ufunuo wa jumla na ufunuo maalum, na kuchunguza kwa makini umuhimu wa kujifunza Fundisho kuhusu Mungu kwa msingi wa uwepo wake, yaani, ushiriki wake wa sasa na hai katika uumbaji, pamoja na umilele wake, asili yake isiyo na ukomo na kutojulikana kwake. Katika somo letu la pili, Mungu kama Muumba: Uangalizi na Utunzaji wa Mungu , tutachunguza ukuu wa mamlaka ya Mungu na uangalizi na utunzaji wake juu ya viumbe vyote na historia. Mungu hufanya mambo yote kulingana na mapenzi yake. Baba Mwenyezi ni mwenye enzi juu ya yote, chanzo cha uhai wote, na mtegemezaji wa yote kupitia Mwana wake, Yesu Kristo. Tutachunguza pia namna utawala wa Mungu unavyoonyeshwa katika uhifadhi na usimamizi wake kwa vitu vyote, na tutaona jinsi ufahamu thabiti wa Kibiblia kuhusu uangalizi na utunzaji wa Mungu unavyoweza kutatua makosa makubwa ya kisasa katika falsafa na theolojia, hususan imani kwamba Mungu ni sawa na uumbaji wake ( pantheism ), imani kwamba Mungu aliyeumba ulimwengu hajihusishi tena na mambo ya ulimwengu ( deism ), mtazamo kwamba matukio yote ya zamani, ya sasa na ya baadaye, yamepangwa tayari na Mungu na kwa sababu hiyo hayawezi kuepukika ( fatalism ), na msimamo kwamba mambo yote hutokea kwa bahati nasibu ( chance ). Tunabadili uelekeo kidogo katika somo letu la tatu, Mungu katika Utatu: Ukuu wa Mungu . Tutaangalia ushahidi wa Kibiblia kuhusu Utatu, Mungu katika nafsi tatu. Maandiko yanafundisha kwamba kuna Mungu mmoja tu, na Mungu huyu mmoja anajifunua kwetu kama Mungu Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Washirika wa Utatu wako katika hali ya umoja, utofauti na usawa, Mungu mmoja wa kweli, Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Mara baada ya kuchunguza Utatu, sasa tutachunguza kwa ufupi sifa za ukuu wa Mungu: hali yake ya kiroho, uzima wake, haiba yake, hali yake ya kutokuwa na ukomo, na asili yake ya kutobadilika.
Made with FlippingBook - Share PDF online