Mungu Mwana – Mwongozo wa Mkufunzi: Capstone Module 10 Swahili Mentor Guide

/ 5

M U N G U M W A N A

Utangulizi wa Moduli

Salamu, katika Jina lenye nguvu la Yesu Kristo! Utambulisho wa Yesu wa Nazareti na kazi yake bila shaka ni somo muhimu zaidi katika tafakari na huduma zote za Kikristo. Ni ukweli usiopingika kwamba haiwezekani kuhudumu katika Jina la Bwana Yesu Kristo ikiwa huduma hiyo imejengwa juu ya maoni na mitazamo potofu na ya aibu kuhusu yeye alikuwa nani (na ni nani), maisha yake yalimaanisha nini, na vile tunavyopaswa kumchukulia leo. Kuwa na ufahamu sahihi juu ya maisha yake, kifo chake, ufufuo wake, kupaa kwake, na kurudi kwake ndio msingi wa kila kitu kwetu. Moduli hii inaangazia maisha na matendo yake makuu. Kuwa mahiri katika maarifa ya kibiblia kuhusu Kristo ndio jukumu hasa la ufuasi na huduma yoyote makini, ya kweli na yenye ufanisi. Katika somo la kwanza, Yesu, Masihi na Bwana wa Wote: Alikuja , tunazingatia umuhimu wa Kanuni ya Imani ya Nikea katika masomo ya Kristolojia. Tutaangalia hasa jinsi Tamko la Imani la Nikea linavyosaidia kuboresha fikra zetu kama wahudumu wa mijini, kuhusiana na kujifunza kwetu maarifa ya kibiblia juu ya Yesu. Hili ni muhimu hasa katika maana ya kutusaidia kuiona kazi ya Kristo katika sura mbili: kunyenyekezwa kwake (yaani, kufanyika kwake mwanadamu na kufa kwake msalabani kwa ajili yetu) na kuinuliwa kwake (kufufuka kwake, kupaa kwake, na tumaini la kurudi kwake katika nguvu). Pia tutaangazia fundisho la kibiblia juu ya asili ya Yesu kama Neno au Logos aliyekuwepo kabla hajaja duniani. Tutazingatia uungu wake pamoja na mafundisho potofu mawili ya kihistoria kuhusu uungu wa Kristo, na tutahitimisha somo letu kwa kutoa maoni juu ya umuhimu wa uungu wa Yesu katika imani na ufuasi wetu. Kisha, somo letu la pili, Yesu, Masihi na Bwana wa Wote: Aliishi , linaangazia ubinadamu wa Kristo. Tutazingatia sababu zake mbili za kuja duniani: kutufunulia utukufu wa Baba na kutukomboa kutoka katika dhambi na nguvu za Shetani. Pia tutaangalia lugha ya Kanuni ya Imani kuhusu ubinadamu wa Yesu, kuchukuliwa kwa mimba yake kwa uweza wa Roho Mtakatifu na kuzaliwa na Bikira Maria, na kuchunguza baadhi ya makosa ya kihistoria yanayohusiana na kukana uungu wa Yesu au ubinadamu wake. Tutamalizia somo hili kwa kuchunguza mambo matatu muhimu ya maisha na huduma ya Yesu duniani. Hayo yanajumuisha utambulisho wake kama “Aliyebatizwa” anayejihusisha na watenda dhambi, Mtangaza Ufalme wa Mungu, akiithibitisha tena haki ya Mungu ya kuutawala uumbaji, na kama Mtumishi wa Yehova Atesekaye ambaye alikuja ili kuitoa nafsi yake iwe fidia kwa ajili ya wengi.

Made with FlippingBook - Share PDF online