Kristo: Mada Kuu Ya Biblia

This is the Swahili edition of Christ: The Theme of the Bible.

KRISTO: MADA KUU YA BIBLIA

NORMAN L. GEISLER

SWAHILI

Kristo: Mada Kuu ya Biblia (Toleo la Pili) Na Norman L. Geisler 2012

KRISTO: MADA KUU YA BIBLIA Toleo la Pili La Norman L. Geisler Kimetolewa na Bastion Books | S.L.P 1033 | Matthews, NC 28106 USA | http://BastionBooks.com Hakimiliki © 2012 Norman L. Geisler. Haki zote zimehifadhiwa. Hairuhusiwi kunakili, kurudufu au kusambaza sehemu yoyote ya kitabu hiki cha kielektroniki kwa namna yoyote na kwa njia yoyote ile, ya kielektroniki au kwa kutumia nakala mango, ikijumuisha kupiga picha, kurekodi kwa njia ya kidijitali au ya analogia, au kwa mfumo wowote wa kuhifadhi na kupata tena taarifa, bila idhini ya maandishi kutoka kwa Norman. L. Geisler au Bastion Books. Hata hivyo, haki zifuatazo zimetolewa kwa mmiliki halali wa kitabu hiki cha kielektroniki pekee: (1) Unaweza kuhifadhi nakala ya faili hii ya kielektroniki katika eneo salama na ambalo halitumiwi na watu wengine kama hifadhi rudufu iwapo nakala yako itapotea kwa sababu ya hitilafu ya kifaa chako au wizi. (2) Unaweza kutunza nakala ya faili hii ya kielektroniki kwenye vifaa viwili vya kielektroniki unavyomiliki. (3) Mnunuzi wa kitabu hiki cha kielektroniki anaweza kuchapisha nakala mango moja na kurudishia nakala hiyo iwapo ile aliyokuwa nayo itatupwa kwa sababu ya uchakavu, au itapotea au kuibiwa. (4) Ni halali na itahesabika kuwa “matumizi sahihi” ikiwa mtu atanukuu maneno yasiyozidi 100 na kutambua chanzo kwa uwazi na kwa namna inayofaa. (5) Wachungaji na walimu wanaweza kununua nakala moja ya kitabu cha kielektroniki na kuwagawia wanafunzi na washirika wao katika mfumo wa kielektroniki pale ambapo kitabu hiki cha kielektroniki kinatumika kama kitabu cha kiada cha kujifunzia na endapo hakuna mapato ya kifedha yanayochukuliwa. Usambazaji wa kitabu hiki cha kielektroniki nje ya mipaka iliyoainishwa hapa juu unaweza kusababisha hatua ya kisheria. Maombi mengine kuhusu matumizi ya nyenzo hii yanaweza kutumwa kwa njia ya posta au kwa barua pepe kupitia anuani ifuatayo: Permissions@BastionBooks.com.

ISBN: 978-1-62932-199-8 Cover Art: Njiani kuelekea Emmau, “. . . Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. . . Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe. …. Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko?” (Luka 24:27, 32). Toleo la kwanza la kitabu hiki lilitolewa na Moody Publishers mwaka 1968, likiwa na kichwa Kristo: Mada Kuu ya Biblia . Kilitolewa tena kikiwa na kichwa To Understand the Bible Look for Jesus (Baker Books: 1979; Wipf and Stock Publishers: 2002). Vitabu katika nakala mango vya toleo la 2002 vinaweza kununuliwa kupitia tovuti ya WipfandStock.com. Toleo hili la Kitabu cha kielektroniki cha mwaka 2012 linajumuisha kiasi kidogo cha maudhui yaliyosasishwa na Dk. Norman Geisler. Shukrani Na kama kawaida, moyo wa mke wangu mzuri Barbara wa kujitoa kwa dhati umeboresha maisha yangu, kitabu hiki na vitabu vyangu vyote. Ninamshukuru Mungu kwa uaminifu wake kwa zaidi ya nusu karne. Pia ningependa kumshukuru Christopher Haun kwa msaada wake muhimu katika uhariri wa muswada wa kitabu hiki.

3

YALIYOMO Dibaji. .........................................................................................................................7 Sura ya 1 | Kristo Ndiye Ufunguo wa Biblia...........................................................9 KRISTO: UFUNGUOWA UVUVIOWA BIBLIA............................................9 KRISTO: UFUNGUOWA KANONI YA BIBLIA. ......................................... 18 KRISTO: UFUNGUOWA UTHIBITISHOWA BIBLIA. ............................. 25 KRISTO: UFUNGUOWA UFASIRI WA BIBLIA.......................................... 33 Sura ya 2 | Kristo katika Agano la Kale................................................................ 34 KRISTO: UTIMILIFU WA UNABII WA KIMASIHI WA AGANO LA KALE............................................................................................................ 35 KRISTO: UTIMILIFU WA UKUHANI WA AGANO LA KALE.................. 41 KRISTO: UTIMILIFU WA SHERIA ZA MAADILI ZA AGANO LA KALE. ................................................................................................................. 47 KRISTO: UTIMILIFU WA AHADI ZA WOKOVU. ..................................... 53 YESU NI YEHOVA (YAHWEH)...................................................................... 55 Sura ya 3 | Kristo katika Maagano Yote Mawili. ................................................. 59 KRISTO: KUFICHWA KATIKA AGANO LA KALE NA KUFUNULIWA KATIKA AGANO JIPYA...................................................... 60 KRISTO: KUTOKA VIVULI VYA AGANO LA KALE HADI UHALISI KATIKA AGANO JIPYA................................................................. 64 KRISTO: KUTABIRIWA KATIKA A.K NA UTIMILIFU KATIKA A.J...... 69 MUHTASARI. ................................................................................................... 76 Sura ya 4 | Kristo katika Kila Sehemu ya Biblia.................................................. 78 KRISTO KAMA MSINGI: MGAWANYOWA MAANDIKO KATIKA SEHEMU NNE . ................................................................................ 78 KRISTO KAMA MSINGI: MGAWANYOWA MAANDIKO KATIKA SEHEMU SITA.................................................................................. 87

5

KRISTO KAMA MSINGI: MGAWANYOWA MAANDIKO KATIKA SEHEMU NANE................................................................................ 93 MGAWANYOWENYE SEHEMU NNE LINGANIFU KATI YA A.K NA A.J ................................................................................................................ 94 Sura ya 5 | Kristo katika Kila Kitabu cha Biblia................................................ 100 TORATI: MSINGI KWA AJILI YA KRISTO................................................ 101 HISTORIA: MAANDALIZI KWA AJILI YA KRISTO................................ 104 USHAIRI: MATAMANIO YA UJIOWA KRISTO. ..................................... 108 UNABII: MATARAJIO YA UJIOWA KRISTO............................................ 111 INJILI: KUDHIHIRISHWA KWA KRISTO. ................................................ 114 MATENDO: UINJILISHAJI AU UENEZAJI HABARI ZA KRISTO......... 117 NYARAKA: TAFSIRI NA MATUMIZI YA UJUMBE WA KRISTO. ......... 117 NYARAKA ZA PAULO: UFAFANUZI KUHUSU KRISTO........................ 118 NYARAKA KWA WATU WOTE: MAHUSIA KATIKA KRISTO............. 122 UFUNUO: MWISHOWA MAMBO YOTE KATIKA KRISTO. ................ 125 Sura ya 6 | Neno la Mungu: Neno-Mtu na Neno-Andishi............................... 127 MFANANO KATI YA NENO HAI NA NENO LILILOANDIKWA. .......... 128 UKUU WA NENO HAI JUU YA NENO LILILOANDIKWA...................... 129 NENO LILILOANDIKWA NI MUHIMU KWA NENO HAI...................... 135 UVUVIO NI MUHIMU KWA UENEZAJI WA UJUMBE WA KRISTO.... 136 UVUVIO NI MUHIMU KWA UFASIRI WA UJUMBE WA KRISTO........ 137 Faharasa................................................................................................................. 142 Bibliografia............................................................................................................ 144 Taarifa zaidi. ......................................................................................................... 145

6

DIBAJ I KITABU HIKI NI MATOKEO YA imani ya dhati kwamba Kristo ndiye ufunguo wa ufasiri wa Biblia, si tu kwa sababu Yeye ni utimilifu wa vivuli na unabii wa Agano la Kale, lakini kwa kuwa Kristo ndiye mada inayounganisha kipindi kizima cha ufunuo wa Maandiko. Kristo alisema mara kadhaa kuwa Yeye ndiye ujumbe mkuu wa Maandiko yote ya Agano la Kale (Lk 24:27, 44; Yh 5:39; Ebr. 10:7; Mt. 5:17). Kitabu hiki ni jaribio la kuchukulia kwa uzito uthibitisho wa Kristo aliposema, “Ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi” (Lk 24:44). Kama tutakavyoona katika kurasa hizi, namna hii ya kuiendea Biblia kwa kumtazama Kristo kama mada yake kuu, haikujikita zaidi katika utafiti wa vivuli, au hata katika unabii wa Agano la Kale, bali ni jaribio la kumwona Kristo kama kiunganishi cha ujumbe unaofunuliwa wa Maandiko Matakatifu kwa ujumla wake. Kristo anawasilishwa kama kiungo kati ya A.K na A.J, maudhui ya kanoni nzima ya Biblia, na mada unganishi ndani ya kila kitabu cha Biblia. Msisitizo uliopo hapa ni juu ya Kristo kama kiini cha umoja wa Biblia kwa kuzingatia sehemu kuu za Maandiko na mgawanyo wake. Kwa namna fulani, huu ni uchunguzi wa Biblia kwa muhtasari katika msingi wa ufunuo wa Kristo. Hakuna madhumuni ya moja kwa moja ya kitheolojia ya kitabu hiki, lakini kinashughulikia maswali ya kitheolojia, kama vile uvuvio wa Biblia na uungu wa Kristo. Hata hivyo, haya yanaibuka kutokana au kwa kuhusiana na mada kuu, ambayo ni kumtambulisha Kristo kama kiini cha ufasiri sahihi wa Biblia. Zaidi ya msukumo mkuu wa kitabu hiki, ambao ni kupendekeza baadhi ya njia za kuyaendea Maandiko kwa kuzingatia ufunuo wa Kristo,

7

pengine suala muhimu zaidi linaloshughulikiwa ni lile la uhusiano kati ya njia hizi mbili za ufunuo wa Mungu – Kristo na Maandiko. Hoja inayotetewa hapa ni kwamba kusudi la ufunuo wa Maandiko ni kumfunua Mwokozi; Biblia ni chombo cha Mungu cha kuwasilisha ujumbe wa Kristo na, kwa sababu hiyo, hatutakiwi kujifunza Biblia kwa kusudi la kuifahamu tu, bali tunapaswa kuichunguza kwa kusudi la kumpata Kristo, kwa kuwa “huyo manabii wote humshuhudia” (Mdo 10:43).

8

SURA YA 1 | KRISTO NDIYE UFUNGUO WA BIBLIA

KRISTO: UFUNGUO WA UVUVIO WA BIBLIA Suala la uvuvio wa Biblia linagusa moja kwa moja mamlaka na uadilifu wa Kristo. Ikiwa Biblia si Neno lenyewe la Mungu, la mwisho na lisiloweza kutanguka, kama Yesu alivyodai, basi mtu hawezi kuweka tumaini katika mojawapo ya mafundisho makuu ya kitheolojia ya Kristo, kwa maana hakuna shaka kwamba msisitizo mmojawapo mkuu wa huduma ya Kristo wa Injili ya Agano Jipya ulikuwa ni uthibitisho wa hakika wa mamlaka ya kimungu ya Agano la Kale. Na kile Yesu alichodai kwa habari ya Agano la Kale, alikiahidi kuhusiana na Agano Jipya. Madai ya Kristo Kuhusu Uvuvio wa Agano la Kale Katika siku za Yesu kulikuwa na njia kadhaa za kurejelea Agano la Kale, na nyingi kati ya hizo zilitumiwa na Yesu katika kuthibitisha uvuvio wa kimungu wa maandiko haya matakatifu. Maandiko Pengine njia ya kawaida ya kurejelea Agano la Kale ilikuwa ni kuyaita “Maandiko.” Neno hili limetumika mara hamsini katika Agano Jipya na linachukua maana ya kiufundi. Katika 2 Timotheo 3:16, tunasoma, “Kila andiko lenye pumzi ya Mungu,” na sehemu nyingine za Agano Jipya zinakubaliana na ufafanuzi huu. Maandiko yanaitwa “matakatifu” (2 Tim. 3:15), na kutambuliwa kama kanoni ya kimungu kwa ajili ya imani na matendo ya mwanadamu (Rum. 15:4; 2 Tim. 3:16-17). Katika suala hili la mwisho, kuna mambo muhimu ya kujifunza katika matumizi ya Yesu ya Maandiko. Aliwapinga viongozi wa kidini (Mafarisayo) wa nyakati zake, akiuliza, “Hamkupata kusoma katika

9

maandiko...?” (Mathayo 21:42). Masadukayo walipomwuliza swali, aliwajibu, “Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu” (Mt. 22:29). Yesu mara nyingi alirejelea ulazima wa Maandiko kutimizwa (taz. Mt. 26:54, 56; Yh 13:18; 17:12). Katika Luka 24:44 Yesu alithibitisha kwamba kila kitu kilichoandikwa juu yake mwenyewe katika Maandiko “lazima kitimie” (rej. mst. 45). Mara nyingi, Kristo alitumia neno “Maandiko” katika ujumla wake, bila kutaja kifungu maalum cha Agano la Kale (taz. Yh 7:38, 42; 19:36; 20:9). Kwa hiyo, Alitumia maneno “kama maandiko yasemavyo” kwa namna fulani sawa na usemi wa sasa “kama Biblia isemanavyo.” Yesu aliyachukulia Maandiko kama ufunuo dhahiri wa Mungu kwa mwanadamu. Alisema, “Maandiko hayawezi kutanguka” (Yh 10:35). Hivyo ndivyo Yesu alivyoyachukulia mamlaka ya kimungu ya maandiko ya Agano la Kale—maandiko ambayo yalikuwa kanoni ya imani, ambayo lazima yatimizwe, na ambayo hayangeweza kutanguka. Imeandikwa Kinachohusishwa kwa karibu na neno “Maandiko” ni kirai “imeandikwa.” Yesu mara nyingi alitumia kirai hiki kuthibitisha mamlaka ya kiungu ya mafundisho yake. Kirai hiki kinapatikana mara tisini na mbili katika Agano Jipya. Kwa kawaida kinatumika kurejelea kifungu fulani cha maandiko; wakati mwingine, hata hivyo, kirai hiki kinachukua umuhimu mpana na kuelekeza wasikilizaji kwenye Agano la Kale katika ujumla wake. Kwa mfano, Yesu alisema, “Lakini kwa nini imeandikwa juu ya Mwana wa Adamu [b] ya kwamba itampasa kuteswa na kudhalilishwa?” (Mk 9:12, TKU). Pengine harejelei hapa kifungu maalum cha Agano la Kale bali mada inayopatikana kote katika Agano la Kale (rej. Mwa. 3:15; Zab. 22; Isa. 53). Mahala pengine Yesu alisema, “… kila kitu kilichoandikwa na manabii kumhusu Mwana wa Adamu kitatimizwa” (Luka 18:31, NEN). Hapa ni dhahiri kwamba kirai hiki kinatumika kurejelea ujumla wa mambo

10

yaliyoandikwa. Katika Luka 21:22, alisema, “Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa .” Kando na marejeo haya ya jumla ya Agano la Kale chini ya kirai “imeandikwa,” kuna nukuu nyingi za watu binafsi ambazo zinadhihirisha kwamba Yesu katika matamko yake alithibitisha mkusanyiko fulani wa maandiko wenye mamlaka, wenye asili ya kimungu, na usioweza kutanguka. Linganisha, kwa mfano, kwamba (1) Yesu alimpinga Shetani kwa nukuu tatu zenye nguvu za Agano la Kale zilizotanguliwa na “ imeandikwa ” (Mt. 4:4, 7, 10). (2) Yesu alilisafisha hekalu kwa mamlaka akisema kwamba “ Imeandikwa , Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala” (Mt. 21:13). (3) Alitamka ole juu ya msaliti wake, kwa msingi wa kwamba “ imeandikwa ” (Mt. 26:24). (4) Yesu alikemea unafiki wa kidini, kwa maneno “kama ilivyoandikwa ” (akinukuu Isa. 29:13 kwenye Marko 7:6). (5) Alithibitisha umasihi wake mwenyewe kwa kutafuta na kusoma “mahali palipoandikwa , Roho wa Bwana yu juu yangu…” (Luka 4:17-18). (6) Yesu alijibu swali la mwanasheria kwa habari ya jinsi ya kuurithi uzima wa milele kwa kusema, “ Imeandikwa nini katika torati?” (Lk 10:26). (7) Aliegemeza mamlaka yake mwenyewe na utambulisho wake pamoja na Mungu kwa msingi wa ukweli kwamba “ imeandikwa katika manabii” (Yh 6:45; taz. 10:34). (8) Yesu hata alithibitisha mamlaka ya kile kilichoandikwa (katika Agano la Kale) licha ya ukweli kwamba viongozi wa kidini wa siku zake walitaka kumwua kwa sababu hiyo hiyo (rej. Lk 20:16-17). Ili Litimie Usemi mwingine uliotumiwa na Yesu kurejelea mamlaka ya Agano la Kale kwa ujumla ni “ili litimie.” Usemi huu unapatikana mara thelathini na tatu katika Agano Jipya. Ingawa kauli hii kwa kawaida inatumiwa kunukuu kifungu fulani cha Agano la Kale, wakati mwingine imetumiwa kwa njia ya jumla zaidi ikirejelea Agano la Kale kwa ujumla. Mfano mzuri wa matumizi ya jumla ya kauli hii unatoka katika Hotuba ya Mlimani

11

(Mt. 5:17), ambapo Yesu alisema, “ Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza .” Baada ya kufufuka kwake, Kristo alitoa uthibitisho sawa na huo kwamba yote yaliyoandikwa kumhusu Yeye katika Torati, Manabii, na Zaburi “ lazima yatimie ” (Luka 24:44). Katika Luka 21:22 Yesu anatazamia wakati ujao ambapo “yote yaliyoandikwa” yatatimizwa . Katika injili ya Mathayo pekee usemi huu umetumika mara kumi na tano. Yesu alisema alibatizwa ili kutimiza haki yote (Mt. 3:15); Alikuja katika ulimwengu huu ili kutimiliza Torati na Manabii, na ni lazima afe, vinginevyo “ Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri?” (Mathayo 26:54). Torati Neno Torati [Sheria] kwa kawaida linatumika kimahususi kumaanisha vitabu vitano vya kwanza vya Agano la Kale, vyenye Torati ya Musa (rej. Lk 2:22; Yh 1:45). Wakati mwingine, hata hivyo, linarejelea Agano la Kale kwa ujumla wake. Katika Mathayo 5:18, kwa mfano, Yesu alisema, “Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka, hata yote yatimie.” Hapa sio tu kwamba Yesu anatangaza wazi mamlaka ya mwisho ya Torati bali anaihusianisha kwa uwazi “Torati” na “Torati na manabii” (mst. 17), yaani, Maandiko yote ya Agano la Kale yanarejelewa kwa ujumla kama Torati. Kuna vifungu vingine ambamo Kristo anathibitisha mamlaka ya kiungu ya Agano la Kale kama Sheria ya Mungu kwa ujumla. Katika Yohana 10:34, kwa mfano, Yesu aliwaambia Wayahudi, “Je! Haikuandikwa katika torati yenu…?” baada ya kuwapa nukuu ya Zaburi 82:6. Hapa neno Torati linajumuisha kitabu cha Zaburi. Mahali pengine, kuna marejeo kama hayo ambapo Yesu anatumia maneno kama “torati yao” (yaani ya Wayahudi, Yh 15:25). Vivyo hivyo, watu wengine katika nyakati za Agano Jipya walilirejelea Agano la Kale kama Sheria ya Wayahudi (rej. Mdo 25:8; Yh 18:31; Yh 12:34).

12

Torati na Manabii Moja ya majina ya kawaida ya Agano la Kale lilikuwa “Torati na Manabii.” Kirai hiki kinapatikana takriban mara kumi na mbili katika Agano Jipya. Yesu alizungumzia “Torati na Manabii” (1) kama kielelezo cha maadili ya kweli (Mt. 7:12), (2) ili kuonyesha dira nzima ya kanoni ya Maandiko ya Agano la Kale (Mt. 11:13), (3) kama yale ambayo alikuja kuyatimiza (Mt. 5:17). Neno la Mungu Kirai kingine kinachoakisi mamlaka kamili ya Maandiko ya Agano la Kale ni “Neno la Mungu.” Agano Jipya linatumia jina hili mara kadhaa likirejelea Agano la Kale kwa jumla wake. Katika Warumi 9:6, kwa mfano, Paulo anasema, “Si kana kwamba neno la Mungu limetanguka”; Waebrania 4:12 inathibitisha kwamba “ neno la Mungu li hai na lina nguvu” (taz. pia 2 Kor. 4:2; Ufu. 1:2). Katika Yohana 10:35, Yesu, akitumia kirai “ neno la Mungu ” sambamba na neno “maandiko,” alithibitisha kwamba “haliwezi kutanguka.” Marko 7:13 inaweka msisitizo zaidi, maana hapa Yesu anaweka tofauti ya wazi kati ya “mapokeo” ya Wayahudi na “neno la Mungu.” Yesu aliwashutumu akisema, “Mkalitangua neno la Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu” (Mt. 15:6). Uchunguzi huu hapo juu unatoa uthibitisho pasina shaka kwamba Yesu wa Injili alithibitisha tena na tena, kama mojawapo ya mikazo mikuu ya huduma Yake, kwamba maandiko matakatifu ya Agano la Kale la Kiyahudi, yaliyotajwa kama “Maandiko,” “Torati”, na “Torati na Manabii,” yalikuwa ni “Neno la Mungu” lisiloweza kutanguka, lisiloharibika na lisilopingika. Kristo ndiye ufunguo wa uvuvio wa Agano la Kale kwa sababu bila shaka alilithibitisha; mtu hawezi kushambulia mamlaka ya Agano la Kale bila kupinga uadilifu wa Kristo.

13

Ahadi ya Kristo Kuhusu Uvuvio wa Agano Jipya Mamlaka ya kiungu ambayo Yesu aliyathibitisha kuhusu Agano la Kale aliyaahidi pia kwa habari ya Agano Jipya. Mara kadha wa kadha Yesu aliwaahidi wanafunzi wake kwamba baada ya kuondoka kwake (kupaa), Roho Mtakatifu angewaongoza katika yale ambayo wangeyazungumza juu yake. Maandiko ya Agano Jipya ni utimilifu wa ahadi hizi. Ni katika mantiki hii Kristo pia ni ufunguo wa uvuvio wa Agano Jipya. Ahadi ya Kristo kwa Wanafunzi Maisha ya Yesu yaliyojaa shughuli nyingi na utume wake wa kiungu havikumpatia nafasi ya kuweka mafundisho yake katika maandishi. Kazi hii aliwaachia wanafunzi wake kwa ahadi kwamba Roho Mtakatifu “atawakumbusha” mambo yote kuhusu Kristo na “kuwaongoza katika kweli yote.” Yesu aliahidi tena na tena mwongozo kuhusiana na yale ambayo wanafunzi walifundisha. Hata wale kumi na wawili walipopewa jukumu la kuhubiri habari za “ufalme wa mbinguni” kwa mara ya kwanza (Mt. 10:7), Yesu aliwaahidi, akisema, “Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.” (mst. 19 20; taz. Lk 12:11-12). Ahadi hiyo hiyo ya msingi pia ilitolewa kwa wale sabini walipopewa mamlaka ya kuhubiri habari za “ufalme wa Mungu” (Lk 10:9). Yesu alisema, “Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi” (Lk 10:16). Baadaye, kwenye Mlima wa Mizeituni, Yesu aliwaahidi tena wanafunzi wake hivi: “…msitafakari kwanza mtakayosema, lakini lo lote mtakalopewa saa ile, lisemeni” (Mk 13:11).

14

Tena baadaye, kwenye Karamu ya Mwisho, Yesu alifafanua ahadi yake kwa wanafunzi kumi na mmoja kwa uwazi zaidi, akisema, “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote , na kuwakumbusha yote niliyowaambia .” (Yh 14:26). Pia aliwaambia, “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote ” (Yh 16:13). Agizo Kuu la Kristo, lililotolewa baada ya kufufuka kwake, lina ahadi ile ile: “Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu” ili “kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi” (Lk 24:49, 47). Katika Mathayo 28:18-19, Yesu anawaagiza wanafunzi kwa “mamlaka yote mbinguni na duniani” kwenda “kufanya mataifa yote kuwa wanafunzi . . . na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi,” akiwaahidi uwepo wake pamoja nao daima katika utekelezaji wa agizo hilo la kufundisha juu yake ( mst . 20). Wanafunzi Wapokea Ahadi ya Kristo Ahadi ya Kristo ya kuwaelekeza wanafunzi katika yale yote ambayo waliyafundisha juu yake ndiyo ufunguo wa mamlaka ya kimungu ya Agano Jipya, na madai ya wanafunzi kuhusu mamlaka hayo ni utimilifu wa ahadi hiyo. Kwa ufupi, 1. Chochote ambacho mitume wa Yesu walifundisha kilitoka kwa Roho Mtakatifu. 2. Agano Jipya ni yale ambayo mitume walifundisha. 3. Kwa hiyo, Agano Jipya lilitokana na Roho Mtakatifu. Ni jambo lililo dhahiri sana kwamba mitume na washirika wao walipokea ahadi ya Kristo katika mafundisho ya maandiko yao yaliyoongozwa na Roho Mtakatifu.

15

Madai ya Kuendeleza Mafundisho ya Kristo Injili ya Luka, kwa mfano, inadai kutoa maelezo sahihi ya yote ambayo “Yesu alianza kufanya na kufundisha” (Mdo 1:1; taz. Lk 1:3-4). Kwa hiyo, kitabu cha Matendo kinatoa kumbukumbu ya yale ambayo Yesu aliendelea kufundisha kupitia wanafunzi wake. Linganisha dai hili na ukweli kwamba kanisa la kwanza lina sifa ya kudumu “katika fundisho la mitume ” (Mdo 2:42), mamlaka ya mwisho ya matamko yao (rej. Mdo 15:22), na kule kuwaombea watu hata kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu kupitia huduma yao (rej. Mdo 8:14-17; 10:45; 19:6). Kulinganisha Maandiko Yao na Maandiko ya Agano la Kale Ni dhahiri zaidi kwamba waandishi wa Agano Jipya walidai kutimizwa kwa ahadi ya Kristo kwa kuweka maandiko yao kwenye kiwango sawa na Maandiko ya Agano la Kale. Hayo ndiyo madai yaliyotolewa katika Waebrania 1:1-2, ambayo inatangaza kwamba Mungu ambaye zamani za kale alinena kwa njia ya manabii, katika siku hizi za mwisho amesema nasi kupitia Mwanawe, ujumbe ambao “…kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia [yaani, mitume]” (Ebr. 2:3). Petro, katika waraka wake wa pili (3:15-16), anaziweka nyaraka za Paulo kwenye fungu moja na “ maandiko mengine ,” na 1 Timotheo 5:18 inarejelea injili ya Luka (10:7) kwa kutumia jina “maandiko.” Kauli Ndani ya Vitabu vya Agano Jipya Zinazoonyesha kuwa Vinamamlaka ya Kimungu Uthibitisho mmoja zaidi kwamba waandishi wa Agano Jipya waliyachukulia maandiko yao kuwa utimilifu wa ahadi ya Kristo unatokana na madai yaliyomo ndani ya vitabu vyao. Kila kitabu kwa namna yake, moja kwa moja au kwa namna isiyo ya moja kwa moja, kinadai kuwa kimeandikwa kwa mamlaka ya kimungu.

16

Injili, kwa mfano, zinajipambanua kama maelezo yenye mamlaka ya utimilifu wa unabii wa Agano la Kale katika maisha ya Kristo (rej. Mt. 1:22; 2:15, 17, 23; 4:14, nk.). Luka alimwandikia Theofilo ili kwamba apate “kujua hakika,” yaani ukweli kuhusu Kristo (1:1, 4). Yohana aliandika ili kwamba wanadamu wapate “kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo...” (20:31), na anaongeza kusema kwamba “ushuhuda wake ni kweli” (21:24). Kitabu cha Matendo, kwa namna isiyo ya moja kwa moja, kinajifafanua kama kumbukumbu inayoendelea ya yale ambayo Yesu alikuwa ameanza kufanya na kufundisha katika Injili (1:1). Nyaraka za Paulo kila moja ilihusisha madai ya kuwa na mamlaka ya kiungu (rej. Rum. 1:3-5; 1 Kor. 14:37; 2 Kor. 1:1-2; Gal. 1:1, 12; Efe. 3:3; Flp. 4:9; 1:1; 1 Tim. 4:11; 2 Tim. 1:13; 4:1; Tit 2:15; Flm 8). Nyaraka za Jumla pia zinadai kuwa na mamlaka ya kimungu (taz. Ebr. 1:1; 2:3; Yak 1:1; 2 Pet 1:1; 2 Pet 3:2; 1 Yoh 1:1; 2 Yoh 5, 7; 3 Yoh 9, 12; Yud 3; Ufu. 22:9, 18-19). Kanisa la Kwanza Lilithibitisha Dai Hili Yesu aliahidi uvuvio, waandishi wa Agano Jipya walitimiziwa ahadi hii, na Kanisa la Kwanza liliithibitisha. Uthibitisho huo ulidhihirika katika ukweli kwamba vitabu vya Agano Jipya: 1. Vilikukubalika kama maandiko yenye mamlaka (2 The. 2:15); 2. Vilisomwa katika makanisa (1 The. 5:27); 3. Vilisambazwa katika makanisa; 4. Vilinukuliwa na waandishi wengine wa Agano Jipya (rej. 2 Pet 3:2-3 na Yud 17-18; 1 Tim. 5:18 na Luka 10:7); na

17

5. Vilikusanywa pamoja na maandiko ya Agano la Kale (2 Pet 3:15). Hivyo basi, Kristo ndiye ufunguo wa uvuvio wa Biblia. Alichodai kuhusu asili na mamlaka kamili ya kimungu ya Agano la Kale, alikiahidi pia kwa habari ya maandiko ya mitume katika Agano Jipya. Uthibitisho wa kwamba hilo ni kweli unaonekana katika uhakika wa kwamba uvuvio ambao Kristo aliuahidi, waandishi wa Agano Jipya waliupokea, na Kanisa la Kwanza liliuthibitisha, yaani, kwamba maandiko ya Agano Jipya yalizingatiwa kuwa na mamlaka ya kimungu sawa na maandiko ya Agano la Kale. KRISTO: UFUNGUO WA KANONI YA BIBLIA Neno kanoni kama linavyotumika kuhusiana na Biblia linamaanisha maandiko ambayo yanachukuliwa kuwa “kanuni” (Kiyunani, Kanon ) au “kaida” ya imani na utendaji. Kwa maana hiyo, “kanoni” ya Maandiko ni vile vitabu ambavyo vimeundwa kwa mamlaka ya kimungu. Kwa maneno mengine, kitabu chenye sifa ya “kikanoni” ni kile ambacho kimevuviwa na Mungu. Sifa ya “kikanoni” au mamlaka ya kimungu ya kitabu yalitolewa au kuamuliwa na Mungu, ambaye alikipa mamlaka hayo. Uhalali wa kikanoni, hata hivyo, ulipaswa kubainishwa au kutambuliwa na watu wa Mungu, ambao waliyakubali na kuyakusanya maandiko hayo. Hili linaibua swali kuhusu vigezo au sifa bainifu za kitabu cha kikanoni. Kanisa lingewezaje kutambua vitabu ambavyo Mungu alikuwa amevivuvia? Kanisa la kwanza mara nyingi lilizingatia vigezo kama vile: 1. Je, kitabu hiki kiliandikwa na mtu wa Mungu? 2. Je, mwandishi alithibitishwa kuwa nabii wa Mungu?

18

3. Je, kinaeleza ukweli kuhusu Mungu (kama anavyojulikana kutokana na mafunuo yaliyotangulia)? 4. Je, kina uwezo wa Mungu (k.m., kujenga)? 5. Je, kilikubaliwa na watu wa Mungu? Kwenye orodha hii kunaweza kuongezwa vigezo vingine vinayoingiliana na baadhi ya hivi (hususan kuhusiana na vitabu vya Agano la Kale), kama: Je, kilithibitishwa na Mwana wa Mungu? Je, Yesu alirejelea au kunukuu kitabu hiki kama kitabu cha kikanoni? Ikiwa ndivyo, basi ufunguo wa uthibitisho wa sifa ya kikanoni unaweza kupatikana katika uthibitisho wa Kristo. Tayari tumejifunza juu ya kile ambacho Yesu alifundisha kuhusu mamlaka ya kimungu ya Agano la Kale kwa ujumla. Iwapo inaweza kubainishwa ni vitabu vipi vilivyounda kanoni ya Agano la Kale ambayo Yesu aliirejelea, basi inaweza pia kuthibitishwa ni nini kilichounda kanoni ambayo Yeye aliidhinisha. Kuna mistari kadhaa yenye ushahidi wa kuthibitisha kwamba kanoni ya Kristo ni sawa na ile ya Agano la Kale la Kiyahudi na la Kiprotestanti la nyakati zetu. Agano la Kale la Kiyahudi la leo lina vitabu ishirini na vinne lakini linafanana na Agano la Kale la Kiprotestanti ambalo lina jumla ya vitabu thelathini na tisa kwa sababu lile la Kiyahudi “linaunganisha” Manabii Wadogo kumi na wawili kuwa kitabu kimoja, kadhalika vitabu vya Wafalme na Samweli [kitabu kimoja], Mambo ya Nyakati [kitabu kimoja] na Ezra-Nehemia [kitabu kimoja]. Wayahudi pia wakati fulani waliorodhesha vitabu vyao kuwa ishirini na viwili, kutokana na Ruthu kuunganishwa na Waamuzi, na Maombolezo na Yeremia, hivyo kuendana na idadi ya herufi katika alfabeti ya Kiebrania. Agano la Kale la Kikatoliki, kwa upande mwingine, lina vitabu vingine saba zaidi (na sehemu nne za vitabu), na kufanya jumla ya vitabu arobaini na sita na sehemu

19

nne za vitabu. Vitabu hivyo vinajulikana kama vitabu vya Apokrifa na vinajumuisha (1) Tobiti; (2) Yudith; (3) Hekima ya Sulemani; (4) Sira; (5) Baruku na Barua ya Yeremia; (6) 1 Wamakabayo; (7) 2 Wamakabayo; (8) Nyongeza ya Esta (10:4-16:24); 11 (9) Sala ya Azaria na Wimbo wa Vijana Watatu (ulioingizwa baada ya Dan. 3:23); (10) Susana (Dan. 13); na (11) Beli na Joka (Dan. 14). Je, Yesu aliviona vitabu hivyo kuwa sehemu ya orodha ya Maandiko yaliyovuviwa? Ushahidi ulio wazi uko kinyume na maoni ya namna hiyo kwa sababu kadhaa. Hata madhehebu ya Kimasihi huko Qumran yalikuwa na vitabu vya Apokrifa lakini ni dhahiri kwamba hayakuvichukulia kuwa na thamani sawa na Maandiko matakatifu. (Milflar Burrows akizungumzia Apokrifa anasema, “Hakuna sababu ya kufikiri kwamba mojawapo ya kazi hizi ziliheshimiwa kama Maandiko Matakatifu” ( More Light on the Dead Sea Scrolls . New York: Viking, 1958, uk. 178). Wasomi wanataja sababu kadhaa tofauti zenye ushahidi unaoonyesha kwamba vitabu vya Apokrifa havikuchukuliwa kama vitabu vya kikanoni huko Qumran: (1) kutokuwepo kwa ufafanuzi wowote juu ya vitabu vya Apokrifa, (2) kushindwa kupata vitabu vyovyote vya Apokrifa vilivyoandikwa kwenye vifaa vya kuandikia vyenye thamani zaidi kama vile ngozi, (3) na hata kutopata vitabu vyovyote vya Apokrifa vilivyoandikwa katika hati zenye herufi maalum (ndefu zaidi), kama ilivyokuwa kwa vitabu vya kikanoni. 2 Ushuhuda wa Yesu Kuhusu Kanoni Kama ilivyokwisha bainishwa, majina ya kawaida zaidi ya kanoni kamili ya Agano la Kale katika siku za Yesu yaliwakilishwa na kirai “Torati na Manabii.” Kirai hiki kinapatikana takribani mara kumi na mbili 1 Katika Agano la Kale la Kiyahudi na la Kiprotestanti, kitabu cha Esta kinaishia na Esta 10:3, na Danieli kinaishia na Dan. 12. 2 Kwa ufafanuzi zaidi wa kipengele hiki ona N. L. Geisler na William Nix, A General Introduction to the Bible (Chicago: Moody, 1988), sura ya 11 au From God to Us , sura ya 8.

20

katika Agano Jipya (taz. Mt. 5:17; Lk. 16:16; Mdo. 24:14), na kila wakati kinakusudiwa kujumuisha Agano la Kale lote (vitabu vyote ishirini na viwili vya Wayahudi au vitabu thelathini na tisa vya Waprotestanti). Katika Mathayo 11:13, upeo wa kirai hiki umeonyeshwa wazi; “Torati na Manabii” inajumuisha maandiko yote yaliyovuviwa tangu Musa hadi Yohana Mbatizaji. Hili bila shaka halifafanui kwa usahihi yaliyomo katika kanoni ya Agano la Kale (hili lazima lithibitishwe kutokana na vyanzo vingine); linachofanya, hata hivyo, ni kubainisha mipaka ya kanoni ya Agano la Kale kama “Torati na Manabii” ya Wayahudi. Kwa hiyo, Agano la Kale lote lilirejelewa katika makundi mawili , Torati na Manabii. 33 Yesu aliziita sehemu hizi mbili “maandiko yote” (Lk 24:27). Kuna ushahidi kutoka kwa jumuiya ya Bahari ya Chumvi huko Qumran kwamba Waesene wakati wa Kristo pia walilirejelea Agano la Kale lote kama Torati na Manabii (Lk 24:27), kama alivyofanya mwandishi wa 2 Wamakabayo (taz. 15:9). Hata hivyo, kulikuwa na mwelekeo wa awali, hata kabla ya siku za Yesu (taz. Dibaji ya Sira, 132 K.K.), wa kuwagawanya Manabii katika sehemu mbili na kupelekea mgawanyo wa sehemu tatu, ambao leo unaitwa Torati, Manabii na Maandiko . Yesu mwenyewe anataja mgawanyo wenye sehemu tatu (Luka 24:44), akiliita Agano la Kale, “Torati ya Musa, na manabii, na zaburi.” Bila kujalisha aina ya mgawanyo, maudhui yalikuwa ni yale yale, kama tutakavyoona hivi punde. Yaliyomo katika Kanoni ya Yesu ya Agano la Kale Josephus, mwanahistoria wa Kiyahudi wa wakati wa Kristo (37-100 B.K), ndiye chanzo bora zaidi kisicho cha kibiblia kuhusiana na yaliyomo katika kanoni ambayo Kristo aliirejelea. Je, kanoni hiyo ilijumuisha vitabu vya Apokrifa au vitabu ishirini na viwili pekee vya Biblia ya Kiebrania ya leo? Jibu la Josephus liko wazi sana:

3 Taz. Manual of Discipline , I, 3; VIII, 15.

21

Maana hatuna wingi wa vitabu miongoni mwetu. . . lakini vitabu ishirini na viwili tu. . . ambavyo vinaaminika kwa haki kuwa ni vya kimungu; na vitano miongoni mwavyo ni vya Musa. . . [2] manabii waliokuja baada ya Musa waliandika yale yaliyofanyika enzi zao katika vitabu kumi na vitatu. [3] Vitabu vinne vilivyosalia vina nyimbo za Mungu, na kanuni kwa ajili ya mwenendo wa maisha ya mwanadamu. (Josephus, Against Apion I, 8). Ushuhuda wa Josephus unatuelimisha kwa sababu, kwa uwazi kabisa, yeye hajumuishi vitabu vyovyote vilivyoandikwa kati ya mwaka 400 K.K. na 100 B.K (enzi yake). Anasema, Ni kweli historia yetu imeandikwa hasa hasa tangu Artashasta [424 K.K.], lakini haijahesabiwa kuwa na mamlaka kama ile iliyoandikwa zamani na wazee wetu, kwa sababu hapakuwa na mfululizo kamili wa manabii tangu wakati huo. ( ibid. ) Yaani, baada ya Malaki, Wayahudi hawakuona kitabu kingine chochote kuwa kimevuviwa. Sasa, kwa kuwa vitabu vya Apokrifa (vilivyoongezwa rasmi kwenye Biblia mwaka 1546 B.K na Kanisa Katoliki la Roma) viliandikwa katika kipindi cha kati ya miaka ya 200 K.K. na 100 B.K, vingekataliwa waziwazi, kwani kwa hakika haviko kwenye orodha ya vitabu ishirini na viwili ambayo Josephus aliitoa. Matumizi ya Yesu ya Agano la Kale yanasuluhisha swali kuhusu yaliyomo katika kanoni bila kuhitaji uthibitisho wowote kutoka kwa vyanzo vya Kiyahudi vya wakati huo. Kwanza, katika Mathayo 23:35 Yesu alifafanua mipaka ya historia iliyovuviwa ya Agano la Kale kuwa ni kati ya mfia imani Habili ​(Mwanzo) na Zekaria (2 Nya. 24:20 au 36:15-16). Hivyo basi, kwa kuwa kulikuwa na wafia imani wengi wa Kiyahudi katika vitabu vya Apokrifa baada ya wakati huo (taz. 2 Wamakabayo 2, 5, 6, 7), ni dhahiri kwamba maelezo ya Yesu hayawahusu hawa kama sehemu ya historia ya Agano la Kale iliyovuviwa. Zaidi ya hayo, katika nukuu na marejeo mengi kutoka katika kila sehemu kuu ya Agano la Kale tangu sura ya kwanza ya

22

Mwanzo (Mwa. 1:27, taz. Mt. 19:4) hadi sura ya mwisho ya Malaki (Mal. 4:5, taz. Mk 9:12), Yesu kamwe hakunukuu au kurejelea vitabu vyovyote vya Apokrifa . Hakunukuu kamwe kitabu chochote isipokuwa vile ishirini na viwili vya Agano la Kale la Kiebrania, ambavyo vinalingana kabisa na vitabu thelathini na tisa vya Agano la Kale la Kiprotestanti. Nukuu za Yesu kutoka katika Torati Yesu katika jibu lake kwa Mafarisayo anarejea andiko la Mwanzo 1:27, “Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke…?” (Mt 19:4-5). Kutoka 16:4, 15 inanukuliwa katika Yohana 6:31: “…kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale.” Yesu anarejea kitabu cha Mambo ya Walawi anapomwambia mwenye ukoma “ukaitoe sadaka kama alivyoamuru Musa.” (Mt. 8:4, ling. na Law. 14:2). Yesu anarejelea andiko la kitabu cha Hesabu katika Yohana 3:14 anaposema, “Kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani...” (taz. Hes. 21:9). Katika vitabu vyote vya Torati, Kumbukumbu la Torati ndicho kitabu ambacho kilinukuliwa zaidi na Yesu. Alimpinga Shetani kwa nukuu tatu za Kumbukumbu la Torati (Mt. 4:4, taz. Kum. 8:3; ​Mt. 4:7, taz. Kum. 6:16; Mt. 4:10, taz. Kum. 6:13). Katika Marko 12:29, Yesu anataja kifungu maarufu cha Kumbukumbu la Torati 6:4 anaposema, “Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja.” Yesu pia alirejelea Kumbukumbu la Torati 24:1-4 kwa habari ya talaka, kadhalika na sheria ya jamaa wa karibu ya Kumbukumbu la Torati 25:5 (taz. Mt. 22:24), na nukuu nyinginezo. Pia, pamoja na ukweli kwamba vitabu vya Agano la Kale kama vile Esta na Wimbo Ulio Bora havijatajwa moja kwa moja na kuthibitishwa na Kristo, hata hivyo vilitimiza vigezo vya kikanoni. Nukuu za Yesu kutoka katika Vitabu vya Manabii Vitabu vya Manabii vilijumuisha sehemu iliyobaki ya Agano la Kale. Vitabu vingi vya kundi hili vilinukuliwa na Yesu. Yoshua na Waamuzi

23

havikunukuliwa na Yesu, lakini Samweli na Wafalme vilinukuliwa. Tendo la Dauli kula “mkate wa wonyesho” (1 Sam. 21:1-6) linatajwa katika Mathayo 12:3-4. Huduma ya Eliya kwa mjane (1 Fal 17) imetajwa katika Luka 4:25. Andiko la Mambo ya Nyakati linarejelewa katika Mathayo 23:35 (taz. 2 Nya. 24:21). Huenda ni Ezra-Nehemia vinavyotajwa katika Yohana 6:31 (taz. Neh. 9:15), “Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale” (ingawa nukuu hii inaweza kuwa ilichukuliwa kutoka Zab. 78:24 au 105:40). Vitabu vya Esta na Ayubu havirejelewi na Yesu moja kwa moja. Hata hivyo, Zaburi ni mojawapo ya vitabu vilivyonukuliwa mara nyingi na Yesu. Alinukuu kutoka Zaburi (1) akiwa na umri wa miaka kumi na miwili (Lk 2:49, taz. Zab. 26:8; 27:4); (2) katika Hotuba ya Mlimani (Mt. 5:35; 7:23, taz. Zab. 48:2; 6:8); (3) alipokuwa akifundisha makutano (Mt. 13:35, taz. Zab. 78:2); (4) alipoililia Yerusalemu (Mt. 23:37, taz. Zab. 91:4); (5) alipolitakasa hekalu (Mt. 21:16, taz. Zab. 8:2); (6) katika kuwajibu Wayahudi (Mt. 21:42, taz. Zab. 118:22-23); (7) wakati wa Karamu ya Mwisho (Mt. 26:30, taz. Zab. 95-98); (8) msalabani (Mt. 27:46, taz. Zab. 22:1); na (9) baada ya kufufuka kwake (Lk 24:44). Kuna uwezekano kwamba Yesu alirejea Mithali mara moja (25:6-7, taz. Lk 14:8-10) lakini hakurejea waziwazi Mhubiri wala Wimbo Ulio Bora. Yesu alitoa nukuu nyingi kutoka katika kitabu cha Isaya (taz. Lk 4:18 ling. na Isa. 61:1; Yh 12:38 ling. na Isa. 53:1). Yeremia sura ya 18 na 19 zimenukuliwa (kupitia Zek. 11:12-13) katika Mathayo 27:9, na Maombolezo (3:30) inarejelewa katika Mathayo 27:30. Ezekieli hakurejelewa waziwazi na Yesu, lakini kurejelea kwake “maji yaliyo hai” katika Yohana 7:38 kunaweza kuwa dokezo la Ezekieli 47:1. Danieli anatajwa waziwazi na Kristo katika Mathayo 24:15 (taz. Dan. 9:27), aliporejelea “chukizo la uharibifu.” Wale Kumi na Wawili (Manabii Wadogo) wamenukuliwa mara kadhaa (taz. Hos 10:8 ling. na Lk 23:30; Zek. 13:7 ling. na Mt. 26:31; Mal. 4:5 ling. na Mt. 17:11). Yesu alinukuu

24

au kurejea takriban vitabu kumi na tano kati ya vitabu ishirini na viwili vya kanoni ya Kiebrania ya Agano la Kale, vikiwemo vitabu kutoka kila sehemu, na mistari kutoka katika sura nyingi kuanzia sura ya kwanza ya Mwanzo hadi sura ya mwisho ya Malaki, lakini hakuna wakati wowote ambapo Yesu alinukuu au kurejea kitabu chochote cha Apokrifa. Kimsingi, kwa kuwa vitabu vya Apokrifa vilijulikana na Wayahudi wa siku za Yesu lakini havikuwa sehemu ya kanoni ambayo wao waliikubali (kama ambavyo Josephus anaonyesha wazi wazi), basi tunaweza, kihalali kabisa, kuhitimisha kwamba Yesu si tu aliviondoa vitabu vya Apokrifa kama sehemu ya kanoni ya Maandiko yaliyovuviwa lakini pia kwa hakika alijitenga navyo kabisa. Kwa ufupi, kanoni ya Kristo, kadhalika kanoni yenye vitabu ishirini na viwili (ishirini na vinne) iliyokubaliwa na Wayahudi wa Palestina wa siku zake, inafanana na vile vitabu thelathini na tisa vya Agano la Kale la Kiprotestanti la siku zetu. KRISTO: UFUNGUO WA UTHIBITISHO WA BIBLIA Si tu kwamba Kristo ndiye ufunguo wa uvuvio na uhalali wa kikanoni wa Biblia, bali pia Yeye ndiye ufunguo wa uthibitisho wa masimulizi ya kihistoria na ya kimiujiza ya Agano la Kale. Matukio mengi makuu ya Agano la Kale ambayo wakosoaji wa Biblia wanayapinga yalithibitishwa na Kristo. Hivyo, mtu atasalia na chaguo la ama kupinga uadilifu wa Kristo wa Injili au kukubali uhalisi wa matukio haya.

Uthibitisho wa Kristo kuhusu Uhalisi wa Kihistoria wa Matukio ya Agano la Kale

Yesu kibinafsi alithibitisha ukweli wa kihistoria kuhusu (1) Adamu na Hawa (Mt. 19:4); (2) Kuuawa kwa Habili ​(Mt. 23:35); (3) Nuhu na gharika (Lk 17:27); (4) Lutu na uharibifu wa Sodoma (Lk 17:29 ); (5) mababa wa Imani: Abrahamu, Isaka na Yakobo (Lk 13:28); (6) Musa na kijiti

25

kilichowaka moto (Lk 20:37); (7) kutangatanga jangwani kwa Israeli (Yh 3:14); (8) hadithi ya Eliya na mjane (Lk 4:25); (9) na ile ya Naamani mwenye ukoma wa Shamu (Lk 4:27); (10) Daudi na hema ya kukutania (Mt. 12:3-4); (11) Sulemani na malkia wa Sheba (Mt. 12:42); (12) Yona na mji wa Ninawi (Mt. 12:41); (13) nabii Danieli (Mt. 24:15); (14) nabii Isaya (Yh 12:38-41). Ni dhahiri kwamba Yesu alithibitisha uhalisi wa kihistoria wa watu hawa na matukio haya kutokana na namna ya moja kwa moja ambayo anawarejelea na mamlaka ya mafundisho ambayo anayajenga kwa kutumia kielelezo cha watu na matukio husika. Kwa mfano, Yesu pale anaposema, “Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi” (Mt. 12:40), kimsingi anathibitisha kuwa matukio yote mawili ni ya kweli kihistoria. Yesu hangetafuta kufafanua ukweli kuhusu kifo na ufufuo wake kwa kutumia hadithi za kubuni kuhusu Yona. Uthibitisho wa Kristo wa Sifa ya Kimuujiza ya Matukio ya Agano la Kale Matukio ya Agano la Kale hayakuzingatiwa tu kuwa ya kihistoria lakini mengi ya matukio hayo yalikuwa ya tabia isiyo ya kawaida. Kwa msingi huo, marejeo ya Yesu yanathibitisha asili ya kimuujiza ya: 1. Uharibifu wa ulimwengu kwa gharika (Lk 17:27); 2. Mke wa Lutu kugeuka nguzo ya chumvi (Lk 17:32); 3. Kijiti kilichowaka moto mbele ya Musa (Lk 20:37); 4. Uponyaji wa Israeli kutokana na kuumwa na nyoka (Yh 3:14); 5. Mana kutoka mbinguni (Yh 6:49);

26

6. Kuponywa kwa Naamani mwenye ukoma (Lk 4:26); 7. Miujiza ya Eliya kwa mjane (Lk 4:25); 8. Kuhifadhiwa kwa Yona ndani ya nyangumi (Mt. 12:41); 9. Unabii wa Danieli (Mt.24:15); 10. Unabii wa Isaya (Yh 12:38-41). Yesu aliyathibitisha haya, kama ambavyo pia alithibitisha kuhusu uwepo wa nafsi ya ibilisi (rej. Mt. 4:1-11), mapepo wasio na idadi (rej. Mk 5:1-13), mazungumzo yake yasiyo ya kawaida pamoja na Musa na Eliya, na miujiza mingi ambayo Yesu aliifanya katika siku zake mwenyewe. Hoja ya Kristo iko wazi: Agano la Kale ni maelezo ya kihistoria ya utendaji usio wa kawaida wa Mungu na watu wake. Baadhi ya wakosoaji wanadai kwamba marejeo ya Yesu kwa watu wa Agano la Kale kama Musa, Daudi, na Isaya hayapaswi kuchukuliwa kuwa uthibitisho wa mhusika kama mwandishi wa kifungu hicho bali kama tendo la kutambua tu uwepo wa kifungu husika. Hata hivyo, nyakati fulani Yesu anamrejelea mwandishi wa kitabu hicho. Kwa mfano, Yesu alirejelea sehemu zote mbili za Isaya (53:1 na 6:10) kama zinazotokana na mtu yule yule Isaya (Yh 12:38, 40), na vile vitabu vitano vya kwanza vya Agano la Kale kama “kitabu cha Musa” (Mk 12:26), “Torati ya Musa” (Lk 24:44), na wakati mwingine kama “Musa” (Lk 16:29; 24:27). Pia alizungumza kuhusu zaburi kama ya Daudi, lakini swali ni kama alitumia majina haya kwa ajili ya kudokeza eneo kinapopatikana kifungu kilichotajwa au kuthibitisha mtu aliyekiandika (au yote mawili). Kuna nyakati Yesu anarejelea kwa uwazi kitabu husika na wala si mtu aliyekiandika. Kwa mfano alipozungumza kuhusu “ kitabu cha Musa” (Mk 12:26), au “yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa” (Lk 24:44), au, “Isaya alitabiri vema.... kama ilivyoandikwa” (Mk 7:6). Hata hivyo, kuna nyakati ambapo Yesu anatofautisha kati

27

ya mwandishi na kitabu chake, kama pale aliposema, “Maana, Daudi mwenyewe asema katika chuo cha Zaburi” (Lk 20:42), au “aliyeandikiwa na Musa katika torati…” (Yh 1:45), au “Daudi katika Roho kumwita Bwana” (Mt. 22:43, taz. mst.42). Katika vifungu hivi na vingine, Yesu alionekana kwenda mbali zaidi ya jina la kitabu na kutoa jina la mwandishi wake. Swali muhimu la kujiuliza kuhusu kila kifungu ni: Ni nini ambacho Yesu anathibitisha? Ikiwa inaweza kuthibitishwa kwamba Yesu anathibitisha wazi wazi au anaashiria moja kwa moja ni nani mwandishi wa kitabu fulani, basi hii hakika itachukuliwa kama uthibitisho wa ukweli huo. Lakini bila kujali jibu la swali hili litakuwaje, hakuna shaka kwamba uthibitisho mwingi na wa kina wa Kristo kuhusu mamlaka, historia na uhalisi wa kanoni ya Kiyahudi ya Maandiko unadhihirisha wazi kwamba alikuwa akifundisha kweli hizi. Uthibitisho au Kukubaliana? Wakosoaji wengine wanadai kwamba Kristo hakuwahi kuthibitisha uvuvio, uhalali au uhalisi wa Agano la Kale hata kidogo. Wanadai kwamba Kristo hakujali kuhusu mambo haya ya urasmi na ya kiufundi hata kidogo, badala yake alichokifanya ni “kukubaliana” na mapokeo ya Kiyahudi yaliyokubaliwa siku hizo. Yaani, Yeye hakuwa akithibitisha, kwa mfano, ukweli wa kihistoria kwamba Yona aliwahi kukaa ndani ya nyangumi, bali alisema, akimaanisha kwamba, “Kama mnavyoamini kwamba Yona alikaa ndani ya nyangumi, kwa hiyo nataka kutumia mapokeo au hekaya hiyo iliyokubalika kukuonyesheni kwamba....” Kulingana na maoni haya, Yesu hakuwa anatoa uthibitisho kuhusu historia, uhalisi, sifa za kikanoni au mamlaka ya Agano la Kale, bali alikuwa akionyesha kukubaliana na masuala haya kama yalivyosadikika nyakati hizo. Janga la nadharia hii “ya kupendeza” ni kwamba inauawa na ushahidi wa kibabe na wa kweli, yaani mambo yanayotokana na sifa na maudhui

28

ya huduma ya Kristo. Kwanza, kwa habari ya mafundisho ya Yesu kuhusu uvuvio wa Agano la Kale, inapaswa kuzingatiwa kwamba mtazamo wowote kama huo wa “kukubaliana” unapingana moja kwa moja na moja ya mada kuu za huduma ya Kristo. Kwa sababu, hili si suala la hapa na pale, au kwamba Yesu alifanya marejeo machache ya Agano la Kale, bali ulikuwa msisitizo wa mara kwa mara na mkuu wa huduma yake. Ikiwa rekodi ya Injili hata inatoa kiini cha kile ambacho Yesu alisema (na kuna ushahidi wa kutosha kwamba inatoa zaidi ya hilo), 4 basi tunajua kwamba Yesu aliamini na kufundisha mamlaka ya kimungu ya Maandiko ya Agano la Kale. Zaidi ya hayo, kuhusu suala la Yesu kulithibitishwa Agano la Kale kama Kanoni, hakuna shaka kwamba Yesu hakukubaliana ilimradi na chochote kilichoaminiwa na Wayahudi . Yesu hakuwahi kusita kukemea maoni ya kidini yaliyokuwepo ambayo hayakuwa ya kweli, kama alivyofanya kwa Wayahudi ambao waliinua “mapokeo” yao juu ya “amri za Mungu” (Mt. 15:1-3). Mara sita katika Hotuba ya Mlimani aliweka kwenye mizani uthibitisho wake na tafsiri za uwongo za Kiyahudi za Agano la Kale, kwa maneno kama vile “Mmesikia kwamba imenenwa... lakini mimi nawaambia” (Mt 5:21-22, 27-28, 31-32, 33-34, 38-39, 43-44). Mara nyingi Yesu aliwaambia, kama katika Mathayo 22:29, “Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.” Alimkemea kiongozi mkubwa wa kidini Nikodemo, akisema, “Je! Wewe u mwalimu wa Israeli, na mambo haya huyafahamu [kuhusu kuzaliwa mara ya pili]?” (Yh 3:10). Yesu pia aliwaambia watu walipokuwa sahihi juu ya Agano la Kale, kama pale alipowaambia Mafarisayo kuhusu zaka, “hayo imewapasa kuyafanya” (Mt. 23:23), au kwa habari ya jibu la mwanasheria kuhusu upendo kuwa amri iliyo kuu zaidi, “Umejibu vema” (Lk 10:28). Kwa upande mwingine, walipokosea tu—ama kimaadili ama kikanuni—Yesu hakusita kuwaita

4 Ona Norman L. Geisler, “New Testament, Historicity of ” katika The Big Book of Christian Apologetics (Baker, 2012).

29

“viongozi vipofu” (Mt. 23:16) au “manabii wa uwongo” (Mt. 7:15). Kristo aliwakemea watu walipokuwa wamekosea, na aliwapongeza walipokuwa sahihi, lakini Yeye mwenyewe hakukaririwa kamwe kuwa alikubaliana na makosa yao—hakika si kwa kosa au upotofu wowote kuhusu Maandiko matakatifu. Bila shaka, wakosoaji wengine wanadai kwamba halikuwa suala la “kukubaliana,” bali ni suala la ukomo wa upeo linalofanya isiwezekane kutumia mamlaka ya Kristo kwa mambo ya kihistoria na nyeti ya Agano la Kale. Wakati fulani inaaminika, kwa mfano, kwamba ujuzi wa Yesu wa mambo haya “yasiyo ya kiroho” ulikuwa mdogo kwa sababu Yeye hakuwa Mungu kweli kweli. Hata hivyo, Yesu alitamka waziwazi kwamba Yeye ni Mungu, akitangaza kwamba Yeye ndiye “MIMI NIKO” wa Agano la Kale (Kut. 3:14) na Mwana wa Mungu Mwenyewe (Mt. 16:16-18; Mk 14:61 62). Madai haya ya uungu, Wayahudi wa zama zake waliokuwa na itikadi kali katika imani yao kwa Mungu mmoja, hawakupata shida kuyatafsiri. Walielewa moja kwa moja alichomaanisha. Yesu aliposema, “Mimi na Baba tu umoja” (Yh 10:30) wakaokota mawe ili wamwue, kwa sababu, walisema, “wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu” ( mst . 33). Vivyo hivyo, Yesu alipomwambia yule mwenye kupooza, “Mwanangu, umesamehewa dhambi zako” (Mk 2:5), waandishi waliuliza swali sahihi kabisa, “Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu?” ( mst . 7). Na Yesu aliposema, “Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko” (Yh 8:58), hakuna ambaye hakuelewa dai lake la uungu (rej. “MIMI NIKO” wa Kutoka 3:14), maana kwa mara nyingine tena waliokota mawe ili wamwue. Kwa ushahidi zaidi kwamba Maandiko kwa ujumla yanafundisha uungu wa Kristo (taz. pia Mt. 26:64 85; Ebr. 1:8). Wengine wamesisitiza kwamba ujuzi wa Kristo uliwekewa mipaka kwa lile tendo lake la kuvaa mwili kama inavyoonyeshwa na ukweli

30

kwamba alisema kuwa hajui wakati wa kuja kwake mara ya pili (Mk 13:32 ); Alionekana kutojua kama mtini ulikuwa na matunda (Mk 11:13); Alisemekana kuwa “akazidi kuendelea katika hekima” (Lk 2:52), na “alijifanya kuwa si kitu” (Flp. 2:7 NEN) alipofanyika mwanadamu. Kujibu hoja hii, inatosha kubainisha kwamba Biblia inathibitisha waziwazi kwamba Kristo, hata katika hali yake ya kuvaa mwili na kuishi kama mwanadamu, hakuwa na mipaka katika yale aliyofundisha. Biblia inasema kwamba Yesu alimwona Nathanaeli chini ya mtini pasipo kuwa katika umbali unaoonekana (Yh 1:48), kwamba “alijua watu wote” na “alijua yaliyomo ndani ya mwanadamu” (Yh 2:24). Yeye alijua sifa za mwanamke wa Samaria (Yh 4:18-19), alijua mapema ni nani angemwamini na ambaye angemsaliti (Yh 6:64), na hata mambo “yote yatakayompata” (Yh 18:4). Alijua kuhusu kifo cha Lazaro kabla ya kuambiwa (Yh 11:14), alijua mapema kwamba Petro atamkana (Mt. 26:34), na juu ya kifo na ufufuo wake mwenyewe (Mk. 9:31), pamoja na matukio yanayohusiana na anguko la Yerusalemu na ujio wake mwenyewe mara ya pili (taz. Mt. 24). Baada ya kuonyesha ujuzi wake kwa wanafunzi katika huduma yake, walikiri, “Sasa tumejua ya kuwa wewe wafahamu mambo yote” (Yh 16:30). Kuhusiana na Yesu kutojua wakati wa kuja kwake mara ya pili (Mk 13:32), bila shaka alilijua hilo kama Mungu; ni katika asili yake kama mwanadamu tu ambapo Baba hakumfunulia (Mdo 1:7). Chochote ambacho Kristo alikiachilia katika Wafilipi 2:7, ni wazi haukuwa uungu wake na sifa ambazo ni sehemu yake (kama vile kujua yote), kwa kuwa Mungu hawezi kubadilika au kuacha kuwa Mungu (Mal. 3:6; Yak 1:17). Kama Mungu-Mtu, Yesu alikuwa na asili mbili tofauti, moja ilikuwa haina kikomo katika maarifa na nyingine ilikuwa na kikomo. Alipojifanya kuwa hana utukufu katika kuvaa kwake mwili (umwilisho), hakujiondoa uungu wake, bali udhihirisho wa nje wa uungu wake na matumizi ya kujitegemea ya uwezo wake wa kiungu. Kama mwanadamu, Yesu aliwekewa mipaka katika ufahamu wake kwa yale ambayo Baba alimfundisha (Mt. 11:27).

31

Katika asili yake ya kibinadamu Yesu alikua katika maarifa kama mtoto (Lk 2:52). Lakini ukweli kwamba hakujua kila kitu kama mwanadamu haukanushi wala kubatilisha mamlaka ya kimungu ya kile alichojua na kufundisha. Na kama tulivyoona, alijua na kufundisha kwamba Yeye alikuwa Mwana wa Mungu na Biblia ni Neno la Mungu. Bila shaka, katika yale ambayo Yesu alifundisha alikuwa chini ya Baba. Yesu alitambua jambo hilo aliposema, “Baba ni mkuu kuliko mimi” (Yh 14:28) na “sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka” (Yh 6:38). Mtume Paulo alifundisha vivyo hivyo alipoandika, “Kichwa cha Kristo ni Mungu” (1Kor. 11:3) na “Mwana mwenyewe naye atatiishwa chini yake yeye aliyemtiishia vitu vyote, ili kwamba Mungu awe yote katika wote” (1Kor. 15:28). Hata hivyo, kuwekwa chini kwa Mwana kwa msingi wa ofisi na utendaji wake hakulazimu wala kumaanisha kuwepo kwa ukomo au mipaka katika ujuzi na asili yake. Mwana yuko chini kwa maana ya ofisi , lakini kwa asili Yeye ni sawa na Baba (Yh 10:30; 5:23; 1:1). Kuwekwa chini kwa Mwana kunatoa funzo tu kwamba kuna utaratibu katika Uungu, si kwamba kuna mipaka yoyote au makosa katika mafundisho ya Kristo. Maana, ni jambo moja kudai kwamba kulikuwa na mapungufu fulani ya kibinadamu katika ujuzi wa kibinadamu wa Yesu na ni jambo jingine kabisa kusema kwamba alikosea katika yale aliyoyafundisha. Kama ambavyo kuvaa mwili kulivyoweka mipaka fulani juu ya uungu wa Kristo usio na kikomo, na hata hivyo hakutenda dhambi kamwe (Ebr. 4:15; 1 Yh 3:5), vivyo hivyo mapungufu yoyote yanayoweza kuhusishwa na ufahamu wake, lazima ithibitishwe kwamba Yeye kamwe hakukosea katika jambo lolote alilofundisha (taz. Yh 8:40, 46). Kwa ufupi, hakuna ushahidi wa kizuizi chochote wala ukomo wowote juu ya ukweli wa yale ambayo Kristo alifundisha, na kwa hakika hakuna makosa katika mafundisho yake.

32

Made with FlippingBook Digital Publishing Software