Misingi ya Utume wa Kikristo, Mwongozo wa Mkufunzi

/ 4 3 3

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

Maono na Msingi wa Kibiblia wa Utume wa Kikristo: Sehemu ya Kwanza

MAELEZO YA MKUFUNZI 1

Karibu katika Mwongozo wa Mkufunzi, Somo la 1 , Maono na Msingi wa Kibiblia wa Utume wa Kikristo: Sehemu ya Kwanza . Lengo kuu la moduli ya Misingi ya Utume wa Kikristo ni kuwasaidia wanafunzi wako kuelewa baadhi ya dhana kuu za kimaandiko kuhusu utume wa Kikristo, na hasa kutafakari juu ya maana ya jiji na umaskini katika uhusiano wake na utume huo. Shauku yetu ni kuwapa wanafunzi mtazamo mpana kuhusu dhana ya utume kama inavyojidhihirisha katika Agano la Kale na Agano Jipya, huku tukizingatia kwa namna ya kipekee asili ya Kristo kama msingi wa kila utume na kila huduma. Dhana ya utume inaendana moja kwa moja na dhana ya ukombozi – kwamba Mungu amekuja katika Kristo kuikomboa dunia kutoka katika utawala wa shetani na hukumu ya dhambi. Kwa namna fulani, hakuna mjadala kamili au sahihi unaoweza kufanyika kuhusu mojawapo ya dhana hizi bila kuhusisha nyingine. Tunataka kupanua maono ya wanafunzi wetu kutoka katika mtazamo wa maisha yao binafsi hadi kupata picha pana ya ukombozi wa ulimwengu mzima. Oswald Chambers anaweka wazi jambo hili: Kuna namna ambayo Ukristo unaelezewa na kuonyeshwa ambayo ni namna ya kihisia tu, dhaifu, na isiyomstahili Mungu; lakini kusema ukweli Ukristo wa Agano Jipya ni kitu ambacho “malaika hutamani kuuchungulia.” Mungu amelipa gharama ya kuukomboa uzao wa wanadamu uliokuwa umeharibika; Si kwamba ataukomboa, bali ameukomboa tayari. Injili ni hiyo hasa—habari njema kuhusu Mungu, kwamba ameukomboa uzao wa wanadamu. “Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake….” Je, Injili, kama inavyoelezewa kwa kawaida, kweli ni habari njema kuhusu Mungu, au ni upotoshaji juu ya Mungu? Haiwezi kuwa habari njema kuhusu Mungu kama haionyeshi kwamba Mungu ameuweka msingi wa maisha ya mwanadamu katika Ukombozi. Ukombozi una maana kubwa zaidi sana kuliko wokovu wangu au wako binafsi – huo ni matokeo tu; uinjilisti bandia huwa na mwelekeo wa kuufanya wokovu binafsi kuwa jambo kuu. Lakini kulingana na Agano Jipya jambo kuu sio kwamba Ukombozi unanigusa mimi tu, bali kwamba unahusika na uzao mzima wa wanadamu. Msalaba si msalaba wa shahidi tu: ni kioo cha asili ya Mungu kilichoelekezwa kwenye tukio moja la kihistoria. Nikihitaji kujua jinsi Mungu alivyo, ninaona jinsi alivyo kupitia Msalaba. Yesu Kristo sio mtu tu anayeniongoza kwa Mungu: ama Yeye ni Mungu, au sina Mungu kabisa. ~Oswald Chambers. Biblical Ethics . (nakala ya kielektroniki la toleo la mwaka 1947). Hants, UK: Marshall, Morgan & Scott: Hants UK, 1996.

 1 Ukurasa 17 Utangulizi wa somo

Made with FlippingBook - Online catalogs