Misingi ya Utume wa Kikristo, Mwongozo wa Mkufunzi

4 3 4 /

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

Wazo la Chambers kwamba msalaba hauwezi kupunguzwa kuwa tu badiliko la maisha binafsi ni wazo muhimu sana kwa maisha yetu ya kiroho, na ni jambo la msingi katika moduli hii. Shauku yetu ni kuwapa wanafunzi mtazamo mpana wa kile ambacho Mungu anakifanya duniani, na ambacho amekuwa akikifanya tangu mwanzo – yaani, kujitwalia watu kutoka katika mataifa ya dunia kwa ajili yake mwenyewe. Utume ni kazi tunayoshirikiana na Mungu katika muktadha huu. Mara kwa mara, utakutana na nukuu katika somo hili ambazo zinagusia vipengele mbalimbali vya “misiolojia” (yaani, somo rasmi la utume wa Kikristo) ambavyo ni muhimu kwa ajili ya majadiliano, lakini havikuingizwa katika muhtasari kwa sababu ya muda. Tafadhali zizingatie nukuu hizi, na uzijadili pamoja na wanafunzi pale inapofaa. Muhtasari wa somo umejikita zaidi kwenye misingi ya kimaandiko na utendaji wake katika utume wa Kikristo, na si katika misiolojia yenyewe . Hivyo basi, usisite kufundisha dhana kuu, maandiko, au maarifa yaliyomo mara kwa mara. Marudio ni msingi wa mkakati wa ufundishaji wa moduli hii (yaani, mbinu ya kitaaluma ya kufundisha). Malengo, maswali ya mapitio, mapitio ya dhana na hoja kuu – vyote hivi vimeundwa ili kumsaidia mwanafunzi “kuchimba” ukweli huo hadi kwenye msingi wa kiini chake kwa njia ya kurudia-rudia wazo moja kuu kwa uendelevu na msisitizo. Usiangalie hili kama tatizo; wanafunzi hasa wale wanaofundishwa kwa maneno wanahitaji marudio ili kuthibitisha na kukazia kweli hizi, na kila mwanafunzi anapaswa kujua ni kweli ipi, dhana ipi, na maarifa gani ni ya muhimu sana kuyajua kwa undani. Rudia haya mambo ya msingi mara kwa mara na yafundishe vya kutosha. Daima tambua pia kwamba, mwanzoni mwa kila somo tunatoa malengo ya somo kwa uwazi na kwa kina. Haya hayapo kwa ajili ya mapambo au kujaza nafasi, bali ni sehemu muhimu ya uzoefu wa kujifunza darasani, na kila utakachosema, kufanya, au kuwaelekeza wanafunzi kukifanya kinapaswa kuyaangazia na kuyasisitiza malengo haya. Yazingatie unapojitayarisha kwa ajili ya kipindi cha darasa, na tafuta maarifa ya ziada, nukuu, na vitabu mbali mbali vyenye maarifa yaliyomo katika malengo hayo. Kadri utakavyoweza kuyasisitiza malengo haya wakati wote wa kipindi cha darasa, ndivyo utakavyoongeza uwezekano wa wanafunzi kuyaelewa kwa kina na kuona ukubwa na uzito wa malengo hayo.

Made with FlippingBook - Online catalogs