Mungu Mwana, Kitabu cha Mwanafunzi, Capstone Module 10 Swahili Student Workbook

6 /

M U N G U M W A N A

Katika somo letu la tatu , Yesu, Masihi na Bwana wa Wote: Alikufa , tutachunguza maana za kitheolojia za unyonge na kifo cha Yesu, kushuka kwake katika utu wake wa kiungu kwa niaba yetu. Tutaangazia kunyenyekezwa kwa Yesu kwa njia ya Umwilisho (incarnation) , maisha na huduma yake, pamoja na kifo chake. Katika kuzingatia dhabihu yake pale Kalvari, tutachunguza baadhi ya mifano ya kihistoria inayosaidia kuelewa kazi yake juu ya msalaba. Hii inahusisha mtazamo wa kifo chake kama fidia kwa ajili yetu, kama upatanisho (utoshelevu wa kimungu) kwa ajili ya dhambi zetu, kama dhabihu mbadala badala yetu, kama ushindi dhidi ya shetani na kifo chenyewe, na kama upatanisho kati ya Mungu na wanadamu. Pia tutachunguza baadhi ya maoni mbadala ya kihistoria kuhusiana na kifo cha Yesu. Haya ni pamoja na kifo chake kama 1) kielelezo cha kiadili, 2) udhihirisho wa upendo wa Mungu, 3) udhihirisho wa haki ya Mungu, 4) ushindi dhidi ya nguvu za uovu na dhambi, na 5) kukidhi heshima ya Mungu. Hatimaye, katika somo letu la nne, Yesu, Masihi na Bwana wa Wote: Alifufuka na Atarudi , tunaanza kwa kuangalia vipengele mbalimbali na maana ya matukio mawili ambayo yanadhihirisha kuinuliwa kwa Kristo. Ufufuo unatumika kama uthibitisho wa Umasihi na uwana wa Yesu, na kupaa kwake kunampa Mwokozi wetu cheo cha hadhi na mamlaka kinachomruhusu kuvijaza vitu vyote kwa utukufu wake. Tunayachunguza haya kwa kuzingatia mafundisho ya kibiblia ya lugha ya Kanuni ya Imani, ambayo itatuwezesha kuelewa nia ya Mungu ya kumwinua Yesu wa Nazareti kuwa mrithi mkuu wa mambo yote kama matokeo ya kifo chake msalabani. Tutahitimisha somo letu kwa kuangalia kauli tatu za mwisho kuhusu Kristo katika Kanuni ya Imani ya Nikea. Tutachunguza kuja kwake katika utukufu, hukumu yake kwa mataifa, na tutazungumzia kwa ufupi utawala wake ujao katika Ufalme wa Mungu. Labda hakuna elimu ya fundisho la kibiblia inayoweza kulinganishwa na msisimko wa kupata ufahamu wa kina, kupitia Biblia na Kanuni ya Imani, juu ya utajiri, ajabu, na siri ya Mwana wa Mungu, Yesu wa Nazareti. Kunyenyekezwa kwake na kupaa kwake ni kiini cha Injili, na kitovu cha kujitoa kwetu, ibada na huduma zetu. Mungu atumie somo hili kuhusu mtu wake mtukufu kukuwezesha kumpenda zaidi na kumtumikia yeye ambaye ndiye pekee aliyepewa ukuu na Baba. Utukufu ni wake!

~ Mchungaji Dr. Don L. Davis

Made with FlippingBook - Online magazine maker