Mungu Roho Mtakatifu, Mwongozo wa Mkufunzi, Capstone Module 14, Swahili Mentor Guide
/ 5
M U N G U R O H O M T A K A T I F U
Utangulizi wa Moduli
Salamu katika Jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu! Kuna kweli chache za kitheolojia katika historia ya Kanisa ambazo zimezua mabishano mengi, kutokubaliana, na mafarakano kama fundisho la Roho Mtakatifu. Kuanzia mabishano ya zamani kuhusu Utatu na fundisho la “ procession ” (yaani fundisho kuhusu nafsi ipi ya Utatu iliipeleka nafsi nyingine kutenda kazi) hadi kutokubaliana kwa siku za leo kuhusiana na ubatizo na karama za Roho Mtakatifu, kuna mengi ambayo yanaweza kutufanya tuliendee somo hili kwa tahadhari; lakini, ninatumai kwa dhati kwamba haitakuwa hivyo. Fundisho la Roho Mtakatifu ni kiini cha uelewa wetu kuhusu asili ya Mungu na namna tunavyoweza kuuishi uwepo wake hai katikati yetu. Roho ametumwa ili kulitia nguvu na kuliongoza Kanisa la Mungu na kuwapa maisha mapya wale wote wanaoitikia kwa imani ujumbe wake kuhusu Yesu. Ni imani yetu kwamba ukweli unaojifunza kuhusu Roho Mtakatifu hautakuwa tu “theolojia rasmi” ambayo inakusaidia kumwelewa Mungu vizuri zaidi, lakini pia itakuwa “theolojia ya vitendo” ambayo inakuwezesha kumtegemea Roho Mtakatifu katika kiwango kinachoongezeka daima kwa kadri unavyoendelea kuhudumu katika Kanisa la Mungu na kushuhudia ulimwenguni. Somo la kwanza, Nafsi ya Roho Mtakatifu , linalenga kufundisha juu ya Mungu Roho kama nafsi ya tatu ya Mungu mmoja wa Utatu. Tutachunguza taswira ya kibiblia ya Roho kama nafsi ya kiungu ambayo ni Mungu na ambayo inatenda kazi katika ufahamu wa kiungu kama Mungu. Pia tutazungumzia uhusiano wa Roho na Baba na Mwana, tukimtazama Roho kama “kifungo cha upendo” kati yao na “zawadi yao ya upendo kwa ulimwengu.” Tutazungumza kuhusu Roho kama “Mpaji wa Uhai” na kuonyesha jinsi majina, vyeo, na alama za Roho katika Maandiko zinavyomwonyesha yeye kama chanzo na mtegemezaji wa maisha ya kimwili na ya kiroho na kama nafsi iliyo kazini ili kuvifanya vitu vyote kuwa vipya. Katika somo letu la pili, Kazi ya Kinabii ya Roho Mtakatifu , tutachunguza asili ya ufunuo wa kinabii, jambo ambalo litatuleta katika ufahamu wa ukweli kwamba Roho ndiye anayelivuvia na kuliangazia Neno la Mungu. Pia tutaona kwamba jukumu la kinabii la Roho linajumuisha huduma yake ya kusadikisha. Yeye ndiye anayeushinda udanganyifu unaosababishwa na dhambi na kutuongoza kwenye toba ya kweli. Kazi ya unabii ya Roho Mtakatifu ni njia ambayo Mungu anajifunua kwetu na njia ambayo anatuwezesha kuamini ufunuo huo.
Made with FlippingBook - Share PDF online