https://user-fNLORqa.cld.bz/Misingi-ya-Utume-wa-Kikristo-Mwongozo-wa-Mkufunzi
/ 3 3 1
MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO
Kuwawezesha Watu kwa ajili ya Uhuru, Ustawi na Haki (muendelezo)
8.1 Maendeleo yanatokana na ufahamu wa kibiblia wa Mungu kama Muumba na Mtawala wa ulimwengu, jambo ambalo linadai kwamba vitu vyote vipatanishwe ndani yake. Maelezo Mungu amewakabidhi wanadamu wajibu wa kuwa mawakili wa uumbaji wake. Uelewa huu unajidhihirisha katika kujali aina tatu pana za mahusiano: mahusiano na Mungu, mahusiano na wengine, na mahusiano na mazingira ( ona Elliston 1989, Transformation, 176). Ingawa mahusiano haya yalivunjwa kwa kuingia kwa dhambi ulimwenguni, utawala wa ufalme wa Mungu sasa unadai urejesho wake. Maendeleo yanatambua kwamba mpaka hapo utimilifu wa Ufalme wa Kristo utakapodhihirishwa, bila shaka kutakuwa na umaskini, unyonyaji, na taabu inayosababishwa na uharibifu ambo dhambi imeusababisha juu ya maeneo haya matatu ya uhusiano. Uelewa huu haupoozeshi wala kukatisha tamaa maendeleo ya kweli ya Kikristo. Ingawa tunaelewa asili ya uovu wa kimaadili ulimwenguni, maendeleo ya kweli yanatafuta kutoa vielelezo vya haki na upatanisho ambavyo vinaakisi haki ya Ufalme wa Kristo. Ufafanuzi • Maendeleo yana nia ya kuwasogeza watu katika uhusiano sahihi na Mungu . Upatanisho wa kweli kati ya watu unategemea upatanisho wao na Mungu. Ingawa “neema ya kawaida” na “mfano wa Mungu” hutoa msingi kwa kiwango fulani cha upatanisho kati ya watu wote, hatimaye aina ya kina na ya kudumu ya upatanisho inaweza kutokea tu kupitia uhusiano sahihi na Mungu kwa njia ya Kristo. Kwa hiyo, kazi ya maendeleo ina shauku ya kusaidia katika kuwaandaa watu kwa ajili ya kuisikia Injili kwa kuishuhudia kweli yake na kuyaishi matokeo yake. • Upatanisho kati ya watu binafsi, matabaka, na tamaduni ni kigezo muhimu. Maendeleo bila shaka yatahusisha njia mpya za kugawana madaraka, kutumia rasilimali, kufanya maamuzi, kutekeleza sera, na kuhusiana na wengine. Kuna haja ya kuvumbua na kuboresha badala ya kuiga tu mifano iliyopo. Ni muhimu sana kuwepo na uwakilishi wa maoni ya watu kutoka matabaka na tamaduni mbalimbali katika kupanga mradi wowote wa maendeleo.
Made with FlippingBook Annual report maker