Theolojia Katika Picha
/ 1 7 1
R e p r e s e n t a n d o l a t e o l o g í a
Kuwawezesha Watu kwa ajili ya Uhuru, Ustawi na Haki (muendelezo)
1.1 Ufalme wa Mungu kama Msingi wa Utume “Misiolojia inazidi sana kuuona Ufalme wa Mungu kama kitovu cha kazi zote za utume” (Verkuyl 1978, 203). Uinjilisti, upandaji makanisa na kazi za maendeleo havitokani na “maandiko ya uthibitisho” machache yaliyojitenga, lakini ni mwitikio wa kudumu kwa mada ya Ufalme ambayo imeenea katika kumbukumbu zote za Maandiko. Ufalme wa Mungu unajumuisha kiini cha utume wa Mungu ( Missio Dei ) ulimwenguni na unatoa msingi wa kuona namna ambavyo shughuli zetu wenyewe zimekusudiwa kuingia katika mpango mzima wa Mungu. 2 1.2 Ufalme kama Urejesho Maandiko yanathibitisha kile ambacho kimedhihirika kupitia maisha na uzoefu wa wanadamu kila mahali; kuna kitu kimeenda vibaya sana katika ulimwengu. Biblia inafundisha kwamba msingi wa tatizo hilo ni wanadamu kukataa utawala wa Mungu. Simulizi ya kitabu cha Mwanzo kuhusiana na Anguko inaonyesha wanadamu kuikataa haki ya Mungu ya kutoa mwelekeo na mipaka kwa maamuzi yao. Tangu wakati huo na kuendelea, uovu ulijaza pengo lililoachwa na kutokuwepo kwa utawala wa upendo wa Mungu. Ulimwengu uliacha kufanya kazi kwa usahihi; kifo kilichukua nafasi ya maisha; ugonjwa badala ya afya; uadui ukachukua nafasi ya urafiki; udhalimu ukachukua nafasi ya ushirikiano; na uhaba ukachukua nafasi ya utele. Mahusiano yote ya wanadamu na Mungu na kati ya mwanadamu na mwandamu yalitiwa sumu na tamaa ya ndani ya kila mtu na kikundi katika jamii kuchukua nafasi ya mamlaka ya Mungu na kujitawala wenyewe. Katika kuitikia kwa neema kwa hali hii, Mungu aliamua kutoutupilia mbali na kuuharibu ulimwengu, bali kuukomboa. Alianzisha mpango wa kuukomboa ulimwengu kutoka katika utumwa wa mamlaka maovu, na kurudisha vitu vyote kwenye ukamilifu chini ya utawala wake wa Kifalme. Katika Maandiko yote mpango huu wa ukombozi unafafanuliwa kama “ Ufalme wa Mungu ,” na ufahamu wa asili yake na njia za kuja kwake unafunuliwa hatua kwa hatua. Johannes Verkuyl anatoa muhtasari wa ujumbe wa Ufalme kwa namna hii: Moyo wa ujumbe wa Agano la Kale na Agano Jipya ni kwamba Mungu. . . anajishughulisha kikamilifu katika kusimamisha tena utawala Wake wa kiukombozi juu ya ulimwengu na wanadamu wote. Katika kuitafuta Israeli, alitutafuta sisi sote na ulimwengu wetu wote, na katika Yesu Kristo aliweka msingi wa Ufalme. Yesu Kristo Masihi “aliyeahidiwa kwa mababa,” ndiye auto basileia 3 : ndani yake Ufalme umekuja, na unakuja kwa njia ya kipekee kabisa na kwa uwazi wa kipekee. Katika mahubiri yake Yesu anafunua utajiri, hazina ya Ufalme huo: upatanisho, msamaha wa dhambi, ushindi juu ya nguvu za mapepo.
1. Ufalme wa Mungu kama
Msingi wa Uinjilisti, Upandaji Makanisa na Maendeleo
2 Tazama George Eldon Ladd (1974, 45 134), kwa utangulizi wa theolojia ya Kibiblia ya Ufalme.
3 Ufalme katika nafsi; yaani, Yule ambaye kwa nafsi yake anadhihirisha kikamilifu utawala wa Mungu.
Made with FlippingBook Digital Publishing Software