Uongofu na Wito, Swahili Module 1 Mwongozo wa Mkufunzi
7 4 /
U O N G O F U & W I T O
mfano wa kuzaliwa upya ili kutuelekeza juu ya ukweli wa maisha mapya kwa njia ya imani ndani yake. Sitiari ya kuzaliwa inazungumza juu ya jenetiki mpya, chanzo kipya kabisa cha nyenzo za uzazi na chimbuko jipya la uhai. Kuzaliwa mara ya pili ni kuingia katika fursa mpya kabisa ya maisha, mwelekeo mpya wa ukuaji, na nafasi mpya za mabadiliko. Ili kuingia katika Ufalme waMungu ni lazima mtu azaliwe mara ya pili, azaliwe kutoka juu, na kuwa mshiriki wa nasaba (DNA) ya Mungu yenyewe. Yesu alipotangaza kwa mara ya kwanza fundisho hili thabiti la ufalme, Nikodemo hakujua kwamba alikuwa anazungumza juu ya Roho Mtakatifu na Neno la Mungu. Akiwa amechanganyikiwa na kufadhaishwa moyoni, Nikodemo aliuliza ni namna gani mtu mzee angeweza kuingia tena ndani ya tumbo la uzazi la mama yake ili kupita upya kwenye njia ya uzazi. Hakuweza kung’amua mafundisho ya msingi ambayo Yesu alikuwa akitoa kuhusu maisha ya kiroho. Ili kupokea uzima wa milele, kuingia katika uhusiano na Mungu, ni lazima mtu azaliwe tena kiroho kwa imani katika Yesu Kristo. Kwa njia ya imani, Mungu hutumia Neno lake kama mbegu ya kiroho ambayo inaumba asili mpya kabisa ndani ya mwamini, asili inayokuja moja kwa moja kutoka kwa Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Neno la Mungu huzaa uongofu katika maisha ya mwamini mpya; linafanya zaidi ya kurekebisha tu maisha ya mtu fulani – linayabadilisha kabisa. Kristo anapoingia moyoni mwa yule aliyeongoka kwa imani, mtu huyu anazaliwa mara ya pili, akiwa na mbegu ya msingi ya uwezo wa kudhihirisha sifa zote za Yule aliyesababisha maisha mapya ndani yake. Hii ndiyo sababu kujitoa kwa Kikristo kamwe hakuwezi kupewa maana finyu ya utii wa nje wa sheria au kufuata kwa nje mapokeo fulani. Kusudi la Mungu ni kuumba na kudhihirisha uhai mpya ndani ya mwamini, huku uzima wa Mungu mwenyewe ukifanyika msingi na chanzo cha utumishi na imani ya Mkristo. Tunachukua sura, uwezo na tabia za wazazi wetu. Ikiwa tumezaliwa na Baba, sisi pia, tutafanana naye, tutaakisi sura yake, na kushiriki maisha yake. Tazama tena Neno jema la Yesu: Yohana 3:3-6: Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. 4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? 5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. 6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. Kinachoweza kuzalisha maisha mapya ndani ya mwamini ni imani pekee katika Neno la Injili ya Yesu Kristo. Wewe je, unaonyesha kufanana na Baba, yaani zile tabia zinazothibitisha kuwa una “macho kama ya Baba yako,” zinazoonyesha kuwa umezaliwa katika familia ya Mungu kwa imani katika Yesu Kristo? “Lazima uzaliwe mara ya pili!”
3
Made with FlippingBook flipbook maker