Wito Halisi: Kumwakilisha Kristo na Ufalme wake kupitia Kanisa

Dibaji

The Urban Ministry Institute ni kituo cha utafiti na maendeleo ya uongozi cha World Impact, shirika la umisheni wa Kikristo lisilofungamana na dhehebu moja lililojikita katika uinjilisti na upandaji wa makanisa katika miji ya Marekani. Taasisi ya (TUMI) iliyoanzishwa Wichita, Kansas mwaka wa 1995, imefadhili kozi, warsha, na matukio ya mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa mijini ndani ya nchi tangu mwaka 1996. Kwa miaka mingi tumerekodi na kufanyia mapitio sehemu kubwa ya nyenzo hizi, na sasa tunazifanya zipatikane kwa wengine ambao wanawaandaa viongozi kwa ajili ya Kanisa la mjini. Mfululizo wa kozi zetu za Misingi ya Huduma unawakilisha sehemu kubwa ya mafunzo yetu ya ana kwa ana yanayotolewa kwa wanafunzi wa ndani hapa Wichita. Tunashukuru na kufurahi kwamba sasa nyenzo hizi zinaweza kupatikana kwako. Tuna uhakika kwamba utaweza kukua sana unapojifunza Neno la Mungu na kuuhusisha ujumbe wake wa haki na neema kwenye maisha na huduma yako. Kwa faida yako binafsi, tumejumuisha nyenzo zetu za kawaida za darasani pamoja na rekodi zake za sauti kwa kila kipindi cha darasa, zikiwa zimewekwa katika mfumo utakao kuwezesha kujisomea mwenyewe. Tumeacha nafasi ya ziada katika nyenzo halisi zilizochapishwa ili uweze kuongeza vidokezo na maoni wakati unaposikiliza rekodi husika. Hili litakusaidia sana unapochunguza zaidi mawazo na mada hizi. Kumbuka, mafunzo katika vipindi hivi yalitolewa katika mazingira ya darasani na kwa njia ya warsha katika Chuo chetu cha Huduma cha Hope School of Ministry. Hii inamaanisha kwamba, ingawa vitabu vilitengenezwa kwa ajili ya wanafunzi ili waweze kufuatilia na kuhusika na zile rekodi kwa karibu, panaweza kuwepo na tofauti kadhaa. Kwa hiyo, unaposhughulika na nyenzo hizi, tafadhali kumbuka kwamba namba za kurasa katika rekodi haziendani na namba za kurasa katika kitabu. Ombi letu la dhati ni kwamba kozi hii ya Mfululizo wa Kozi za Misingi ya Huduma itathibitika kuwa ya baraka na yenye kukutia moyo katika mwenendo na huduma yako kwa Kristo. Kwa hiyo, Bwana na aitumie kozi hii kuongeza uelewa wako wa Neno lake, ili kwamba ujazwe maarifa na kuandaliwa kutimiza kazi aliyonayo kwa ajili yako katika huduma ya Ufalme.

7

Made with FlippingBook Digital Publishing Software