https://user-fNLORqa.cld.bz/Misingi-ya-Utume-wa-Kikristo-Mwongozo-wa-Mkufunzi

/ 1 1 7

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

kukamilishwa. Yesu sasa amekuwa chanzo na uzima wa Kanisa, bibi-arusi wake mpya, na Yohana Mbatizaji, mtangulizi wake, amekuwa rafiki wa bwana-arusi. Siri ya mwili sasa imefunuliwa kupitia mitume na manabii, kwamba Mataifa ni warithi pamoja na Wayahudi katika ahadi ya agano jipya la Mungu, na kupitia hilo, wanakaribishwa kama washiriki wa jamii mpya ya watu wa Mungu na bibi arusi wa Kristo. Mapenzi ya kiungu yatakamilika kwa kushuka kwa Yerusalemu Mpya kutoka mbinguni, makao ya Mungu na watu wake, ambao watajitambulisha kikamilifu na Kristo, bwana-arusi, kwa kubadilishwa na kufanana naye, kuwa warithi pamoja naye, na kukaa katika uwepo wake milele kama watawala pamoja naye. Kwa hiyo, utume ni kazi ya kueneza ujumbe huu wa Mungu kuchagua watu kutoka katika mataifa yote, ambao kwa imani katika Yesu Kristo wanafanyika washiriki wa jamii ya ufalme wake, ambao wataishi pamoja naye milele. Taswira ya Utume kama Vita vya Milki labda ndiyo taswira ya utume yenye nguvu zaidi katika Maandiko, na huanza na utawala mkuu wa Mungu Yahweh kama muumbaji na mtegemezaji wa yote. Utawala wa Mungu ulipingwa katika “siri ya kuasi” (yaani, uasi wa kishetani huko mbinguni), ambao ulisababisha majaribu na anguko la wanadamu, na laana kwa uumbaji. Mungu aliweka uadui kati ya Uzao wa mwanamke na nyoka, na kwa ukuu wake na neema yake akaahidi kukomesha uasi huo kupitia Uzao wa mwanamke. Kama matokeo ya Anguko, ulimwengu uko vitani, na Mungu amejitangaza kuwa anapigana na nyoka na wale walio upande wake. Mungu alijidhihirisha kuwa Shujaa wa kiungu katika mapambano yake dhidi ya uovu uliofananishwa na mto na bahari, kushindwa kwa Farao na majeshi yake, na mataifa ya Kanaani. Kwa namna isiyo tarajiwa, Mungu pia alilazimika kupigana na watu wake mwenyewe kwa sababu ya kutotii kwao na uasi wao. Zaidi ya hayo, manabii wa Israeli walimfunua Mungu kama Shujaa wa kiungu ambaye hatimaye kupitia Masihi wake angeharibu uovu wote mara moja, milele. Utawala huu wa Kimasihi umewekwa ndani ya Yesu, ambaye katika kuzaliwa kwake, mafundisho, miujiza, kufukuza pepo, matendo yake, kifo chake, na ufufuo wake ameuleta Ufalme wa Mungu. Ufalme uko “tayari” na “bado;” tayari umekuja kupitia Yesu ambaye ametimiza ahadi ya Kimasihi, lakini utakamilika wakati wa Kuja kwake Mara ya Pili. Leo katika ulimwengu huu na katika zama zetu, Kanisa la Yesu Kristo ni ishara na kionjo cha Ufalme uliopo. Roho Mtakatifu anakaa ndani ya Kanisa kama dhamana (arabuni) ya urithi kamili ujao. Kanisa sasa, kama wakala wa Ufalme na naibu wa Kristo, limepewa mamlaka ya kutangaza na kudhihirisha ushindi wa Kristo dhidi ya Shetani na laana. Umisheni unatangaza kwamba katika zama hizi Mungu anaimarisha utawala wake leo juu ya ulimwengu wake katika Yesu Kristo, na kupitia wakala wake, Kanisa.

2

Made with FlippingBook Annual report maker