https://user-fNLORqa.cld.bz/Misingi-ya-Utume-wa-Kikristo-Mwongozo-wa-Mkufunzi

2 0 /

MISINGI YA UTUME WA KIKRISTO

tuache kuimba nyimbo zetu, tugeuze vichwa vyetu, na kutufanya tuvutiwe na kuanza kufikiria jinsi hadithi itakavyokuwa na mwisho wake utakuwaje. Kwa maana halisi, sisi sio tu viumbe wenye akili timamu, bali kama Socrates alivyowai kusema, (na kimsingi zaidi) sisi ni viumbe wanaosimulia hadithi; tunajielewa kulingana na hadithi tunazothamini, tunazosimulia, na hadhithi tunazojihusisha nazo. Hadithi ambazo tunazungumza juu ya taifa letu, familia zetu, na utu wetu ndio msingi wa uelewa wetu kuhusu utu wetu (yaani sisi ni nani), na pia ni msingi wa mambo tunayoshikamana nayo. Wahusika, mada, ploti (mtiririko wa matukio), na mandhari ya hadithi tunazosimulia hutengeneza mitazamo yetu wenyewe kuhusu maana ya ukweli, uadilifu na maadili ambayo tunakumbatia na kuyachukulia kama kanuni zinazoongoza maisha yetu. Kwa kweli, si jambo gumu kupata mtu, familia, ukoo, utamaduni, au taifa ambalo linajielewa kulingana na hadithi zao kuu ambazo zinabeba msingi wa falsafa zao, zinajenga maoni yao kuhusu historia, na kuunda mafungamano yao ya kijamii, kitamaduni, na kitaifa. Kwa njia fulani, tunaishi kulingana na hadithi ambazo tunasimulia, tunaamini, na ambazo tumewekea msingi wa maisha yetu. Msisitizo huu wa kawaida wa kijamii na kibinafsi juu ya jukumu la hadithi (bila kujali kwamba tunaziona kuwa hadhithi za kubuni au za kweli kihistoria) unaonekana kupotea kwa njia nyingi miongoni mwa wanaume na wanawake wengi wa Kanisa la leo. Katika makanisa yetu mengi tunaweka mkazo juu ya kweli za kinadharia, juu ya kanuni za imani na matamko ya imani, juu ya muhtasari mzuri na mfupi wa hadithi za Injili zilizochekechwa ili kupata sentensi chache ambazo ni rahisi kuhubiri au kufundisha ndani ya muda mfupi na hata kuzikariri kwa urahisi zaidi. Ingawa aina hii ya matumizi ya theolojia na kweli ya Kikristo inaweza kuwa na manufaa katika baadhi ya mahubiri na mafundisho, hasa kwa watu wachanga katika imani, kiini na msingi wa Injili umejikita katika hadithi ya Yesu ambayo haijafupishwa kwa “muhtasari safi.” Badala yake, imesimuliwa vyema kwa shauku, furaha, na mshangao tunapoangazia hadithi ya ajabu ya upendo mkamilifu wa Mungu unaoonyeshwa katika unyenyekevu wa ajabu wa Mwanawe kupitia tendo la kuvaa mwili, upendo wa kina ulioonyeshwa msalabani Kalvari, na ushindi mkuu ulioonyeshwa katika ufufuo wake na kupaa kwake mkono wa kuume wa Baba. Hakika, nguvu na neema ya Yesu Kristo haiwezi kupatikana katika kanuni na matamko ya imani peke yake; ni lazima ielezewe na kuigizwa tena na tena katika Neno na sakramenti. Ni asili ya imani ya Kikristo kusimulia hadithi hii na kuisimulia tena na tena. Tunaokolewa kwa kuing’ang’ania Injili na kutengeneza maisha yetu kupitia “Habari Njema” ambayo imekuwa “habari njema ya furaha kuu,” angalau kwa wale wanaoamini.

1

Made with FlippingBook Annual report maker