Kristo: Mada Kuu Ya Biblia

SURA YA 5 | KRISTO KATIKA KILA KITABU CHA BIBLIA

SURA HII NI KILELE cha yote yaliyotangulia. Kwanza, Kristo ameelezewa kama ufunguo wa uvuvio na ufasiri wa Biblia nzima (sura ya 1). Baada ya hili likafuata jaribio la kubainisha njia mbalimbali ambazo Kristo ni mada kuu ya Agano la Kale (sura ya 2). Kisha Kristo akawasilishwa kama kiungo kati ya A.K na A.J, akihusianisha moja kwa jingine kama matarajio yanavyohusiana na utimilifu (sura ya 3). Katika sura iliyopita (sura ya 4), Kristo alihusishwa na njia mbalimbali za kugawanya Biblia. Katika sura hii Kristo atawasilishwa kama mada ya msingi ya kila kitabu cha Biblia. Bila shaka, itakuwa ni kwenda mbali sana kudokeza kwamba Kristo ndiye mada iliyo wazi au kuu ya kila kitabu kimoja katika Biblia, kwa sababu hili linaonekana wazi kuwa si sahihi. Kwa kuwa baadhi ya vitabu vina mada ya kihistoria (kama Ezra au Esta) au mada ya kibinafsi (kama Filemoni) au mada ya kimaadili (kama manabii wengi), ni urohoshaji tu usio na msingi unaoweza kufanya vitabu hivyo vieleweke kimakosa kuwa Kristo ndiye mada yake kuu. Hata hivyo, kwa kuzingatia madai ya wazi ya Yesu—kama yalivyofafanuliwa katika sura zilizotangulia—mtu hangekuwa anaenda mbali sana kwa kumfanya Kristo aonekane kuwa ni mada iliyo nyuma ya Maandiko yote. Wakati mwingine mada hii ya Kristo inakuwa sanjari na mada kuu ya kitabu husika na wakati mwingine sio, lakini inakuwepo hapo kila wakati. Yaani, kila kitabu kimoja kimoja katika Maandiko kimechangia nyuzi fulani za kweli kwa ujumbe mkuu. Kwa kuwa Biblia nzima inazungumza juu ya Kristo, basi sehemu zote lazima zichangie kwa namna fulani katika ujumbe huo.

100

Made with FlippingBook Digital Publishing Software