Theology of the Church, Swahili Mentor Guide

/ 2 2 3

THEOLOJIA YA KANISA

Sehemu hii ya video imejikita katika kuelewa maana ya wokovu. Kitheolojia ni muhimu kwamba wanafunzi waweze kueleza kwa nini tunahitaji kuokolewa (dhambi imetutenganisha na Mungu), njia inayokusudiwa ambayo kwayo tunaokolewa (kwa kuungamanishwa na Kristo katika kifo na ufufuo wake), na maana ya kibiblia ya wokovu (kuungamanishwa na watu wa Mungu wanaorithi Ufalme wake na ahadi zake). Ni muhimu kwa ufahamu sahihi wa wokovu kufahamu kwamba muungano na Kristo hauwezi kutenganishwa na suala la kuingizwa katika Kanisa. Fundisho la maandiko liko wazi kabisa juu ya jambo hili. [Angalia Nyongeza ya Somo hili lenye kichwa “Wokovu Kama Kujiunga na Watu wa Mungu]. Kuokolewa na Kristo ni kuunganishwa na mwili wake, yaani kanisa ambao yeye ndiye kichwa chake (Kol. 1:18) na kushiriki katika mpango wake wa kuwaita na kuwakomboa watu kutoka katika dunia (2Kor. 6:15-16; Tito 2:18 na 14; Ebr. 1:18) na ambao watafanyika aina mpya ya jamii ya wanadamu (1 Kor. 15:45-49). Maneno ya kuaga ya Kristo kwa wanafunzi wake hayakuwa tu kuhubiri Habari Njema kwa kila kiumbe bali pia kuwabatiza (Mt. 28:19), ambayo ni ishara ya wazi ya nje ambayo kwayo watu binafsi wanatambulishwa pamoja na watu wa Mungu daima. Hatimaye, ni muhimu kwa wanafunzi kufahamu kwamba, kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli wakati wa Kutoka ambao walikuwa wameokolewa (kuwekwa huru kutoka utumwani Misri), waliokuwa wakiokolewa (wakisafiri kwenda hadi Nchi ya Ahadi), na ambao wangeokolewa (kushiriki katika urejesho wa vitu vyote wakati hekalu la Bwana lilipoinuliwa kama lililo kuu kati ya milima), wokovu wetu pia ni ukweli uliotimizwa, tumaini linaloendelea, na tumaini la wakati ujao. Kwa sababu hiyo Maandiko yanaturejelea sisi kama wale “wanaookolewa” (1 Kor. 1:18; 2 Kor. 2:15); yanazungumza juu ya “tumaini la wokovu” (1 The. 5:8), juu ya wokovu wetu kuwa “karibu sasa kuliko tulipoanza kuamini” (Rum. 13:11); wokovu kama kitu ambacho “kitarithiwa” (Ebr. 1:14) na kama kitu ambacho Kristo atatuletea atakaporudi (Ebr. 9:28). Ijapokuwa Maandiko yanarejelea kwa uwazi wokovu kuwa ni tukio “lililopita” lililohakikishwa na Kristo msalabani (Efe. 2:5, Tito 3:4 5), na kama “uhalisia wa sasa unaotokea kwa wale wanaoamini” (1 Kor. 1:18; 2 Kor. 6:2), sikuzote maandiko yanatazamia kwa hamu maana kuu ya wokovu kama tendo linalokuja kwetu kupitia kurudi kwa Kristo duniani.

 11 Ukurasa 25 Muhtasari wa Sehemu ya 2

Made with FlippingBook - Share PDF online